Friday, November 21, 2014

Sikinde, Kopa kuwasha moto Swahili Arts Carnival



NA MWANDISHI WETU
BENDI Kongwe ya muziki wa dansi, Sikinde pamoja na Malkia wa muziki wa Taarab Afrika Mashariki, Khadija Kopa ni miongoni mwa wanamuziki watakatoa burudani kwenye Tamasha la Sanaa na Ubunifu wa Mswahili (Swahili Arts and Creative Carnival).
Akizungumza na mtandao wa jamii,  mmoja wa waratibu wa tamasha hilo, Ahadi Kakore amesema kuwa Sikinde ni miongoni mwa bendi zinazopiga muziki wa Kiswahili asilia ndiyo maana wameamua kuiweka kuwa bendi rasmi ya dansi ya tamasha hilo.
Aliongeza kuwa kwa upande wa Khadija Kopa naye atakuwa na bendi yake ya Ogopa Kopa Classic ambayo siku hiyo imeahidi kuimba nyimbo zake mpya ambazo nyingi zitaimbwa kwa mara ya kwanza siku hiyo.
“Mbali ya kuwepo kwa burudani hizo za muziki lakini haina maana kuwa ndiyo tumefunga mlango kwamba hatutakuwa na wasanii wengine ila bado tupo kwenye mazungumzo na wanamuziki nyota wa kizazi kipya kwani tumelenga kuwafikia watu wa rika zote.
“Pamoja na burudani za watu wazima pia watoto nao hawajaachwa nyuma kwa sababu kutakuwa na michezo maalum kwa watoto na zawadi nyingi zipo kwa ajili yao ili kuhakikisha wanafurahia siku hiyo.
Mbali na muziki, burudani nyingine zitakazokuwepo siku hiyo ni maonyesho ya filamu za Kiswahili, maonyesho ya mavazi, vyakula, nyama choma, vinywaji pamoja na michezo ya watoto na maonyesho ya bidhaa za wajasiriamali na watu 1,000 wa kwanza watapata zawadi langoni,” alisema Kakore.
Swahili Arts and Creative Carnival linatarajiwa litafanyika Novemba 29 mwaka huu kwenye viwanja vya Posta, Kijitonyama jijini Dar es Salaam huku likiwalenga watu wazima na watoto kuanzia saa 4:00 asubihi hadi usiku wa manane.
Tamasha hilo limeandaliwa na Kampuni ya Swahili Arts & Creative Carnival kwa kushirikiana na Hildelly Solution na Wazalendo Bright Media kwa udhamini wa Amo Transport Solutions, Coca Cola, Tigo, Oriflem, Chibuku, Global Publishers, CTN na Sibuka TV. 

Tuesday, November 18, 2014

IGP MANGU AONGEZA ASKARI KITETO


E88A9486
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini,IGP Ernest Mangu akimsikiliza Diwani wa Kata ya Matui Wilayani Kiteto Bw.Athuman Kidawa wakati alipofanya ziara wilayani humo kufuatia kuwepo kwa migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji iliyosababisha kutokea mapigano yaliyosababisha kutokea kwa  vifo.kushoto ni Afisa tarafa wa Matui Bw.Eliakimu Ndelekwa.(Picha na Frank Geofray-Jeshi la Polisi)E88A9514
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini,IGP Ernest Mangu akizungumza na wananchi  wa Kata ya Matui Wilayani Kiteto wakati alipofanya ziara wilayani humo kufuatia kuwepo kwa migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji iliyosababisha kutokea mapigano yaliyosababisha kutokea kwa  vifo. (Picha na Frank Geofray-Jeshi la Polisi)E88A9421
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini,IGP Ernest Mangu akizungumza na Mtendaji wa Kijiji cha Chekanao, Kata ya Kiperesa , Wilayani Kiteto Bw.Omar Ndee (kulia) wakati alipofanya ziara wilayani humo kufuatia kuwepo kwa migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji iliyosababisha kutokea mapigano yaliyosababisha kutokea kwa vifo.Katikati ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Deusdedit Nsimike pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji hicho Bw.Japhet Chafu (Picha na Frank Geofray-Jeshi la Polisi)
Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi, Kiteto.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Ernest Mangu ameahidi kuongeza idadi ya Askari katika kijiji cha Chekanao, kata ya Kiperesa wilayani Kiteto Mkoani Manyara kufuatia wananchi katika kijiji hicho kujitolea nyumba kwa ajili ya kuishi Askari kwa lengo la kuimarisha usalama katika maeneo yao kufuatia kuwepo kwa migogoro ya ardhi inayosababisha kutokea kwa mauaji.
IGP Mangu aliyasema hayo jana wakati alipokuwa katika ziara Wilayani Kiteto ya kujionea uharibifu uliojitokeza pamoja na kutafuta ufumbuzi wa migogoro hiyo iliyopelekea kutokea kwa vifo vya wakulima na wafugaji hivi karibuni katika wilaya hiyo ambapo watu kadhaa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kutokana na vurugu hizo.
Alisema kufuatia kuwepo kwa umbali mrefu wa kituo cha Polisi na kijiji hicho atahakikisha askari wa kudumu wanakuwepo ili kushirikiana na wananchi katika kuwabaini wahalifu wanaofanya vurugu na kuendeleza migogoro hiyo ambapo wananchi nao waliahidi kujenga kituo cha Polisi.
Kwa upande wake Mtendaji wa Kijiji cha Chekanao Bw.Omar Ndee alisema wamekuwa wakipata shida kutokana na umbali mrefu wa kituo cha Polisi jambo ambalo limekuwa likifanya kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu vinavyochangiwa na migogoro ya ardhi katika wilaya ya Kiteto.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji hicho Japhet Chafu alilishukuru Jeshi la Polisi kwa kuimarisha usalama kijijini hapo tangu kutokea kwa mauji ya wakulima na wafungaji ambapo alibainisha kuwa bila kuwepo wao hali ingekuwa mbaya zaidi kutokana na kutokuwepo na muafaka baina ya wakulima na wafugaji.
“IGP hawa askari wako wasingekuwepo hapa usingekuta mtu lakini tunawashukuru sana hawa askari kwa kuwa hivi sasa hali ya usalama imerejea na hata shambani tumeanza kwenda” Alisema Bw.Chafu.
IGP Ernest Mangu alitumia ziara hiyo kuzungumza na Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, Wakaguzi wa Tarafa pamoja na Askari Kata ili kutafuta ufumbuzi wa migogoro hiyo na kuimarisha hali ya ulinzi na usalama.
(Picha na habari kwa hisani ya Fullshangweblog.com)

Sikinde, Khadija Kopa jukwaani Nov.29

NA MWANDISHI WETU
MALKIA wa mipasho Tanzania, Khadija Kopa  na Bendi ya Sikinde ‘Ngpma ya Ukae’ wanatarajia kupanda kwenye jukwaa moja katika tamasha la sanaa na ubunifu la Mswahili maarufu kama Swahili Arts & Creative Carnival 2014, litakalofanyika Novemba 29 mwaka huu, kwenye Viwanja vya Posta Kinjitonyama jijini Dar es Salaam. 
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mratibu wa tamasha hilo, Ahadi Kakore amesema kuwa wameongeza bendi hiyo pamoja na Khadija Kopa kutokana na uwezo wao katika kazi na pia wamefanikiwa kuupeleka muziki wa Tanzania mbele.
“Maandalizi yanakwenda vizuri kwa sehemu kubwa hivyo niwaambie wapenzi wa burudani kwamba tamasha lao kwa ajili yao limeshawafikia.
“Pamoja na uwepo wa burudani ya muziki lakini  burudani nyingine zitakazopamba ni ni maonyesho ya filamu za Kiswahili, vyakula, maonyesho ya mavazi, nyama choma, vinywaji pamoja na michezo ya watoto huku tamasha likitarajiwa kuanza saa 5:00 asubuhi hadi usiku wa manane na watu 500 wa kwanza watapata zawadi langoni,” alisema Kakore.
Tamasha hilo limeandaliwa na Kampuni ya Swahili Arts & Creative Carnival kwa kushirikiana na Hildelly Solution na Wazalendo Bright Media kwa udhamini wa Amo Transport Solutions, Coca Cola, Tigo, Oriflem, Chibuku, Global Publishers, CTN na Sibuka TV.

Monday, November 3, 2014

sera ya elimu kufutwa

Serikali imesema wakati wowote kuanzia sasa, itaifuta sera ya elimu inayotumika nchini kutokana na kukamilika kwa mchakato wa uanzishwaji sera mpya ambayo imepangwa kuzinduliwa na Rais Jakaya Kikwete, mwezi huu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome, alisema sera hiyo tayari imepitishwa baada ya kujadiliwa na vikao vya Baraza la Mawaziri.

Akizungumza jana katika uzinduzi wa Chuo Kikuu kipya cha  Mwenge (MWECAU) kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki kilichopo nje kidogo ya mji wa Moshi, Profesa Mchome alisema uamuzi huo wa Wizara hiyo umelenga kuhakikisha kwamba sekta hiyo inakua na kukidhi mahitaji na matarajio ya jamii ndani na nje ya nchi.

“Tumeanza kuboresha elimu yetu kwa kuangalia eneo la mifumo ya kisera na kimsingi, tumefumua sera inayotumika. Huko tumeangalia mwelekeo wa sasa wa dunia inavyokwenda, mabadiliko ya sayansi na teknolojia, viwango na vigezo vya ubora wa elimu inayotolewa,” alisema.

Alisema mambo mengine yaliyohakikiwa wakati wa uandaaji wa sera mpya ni njia za kuwapata wahitimu wenye elimu bora na yenye viwango ambavyo vimebainishwa na kuwekwa kisera ili kuepusha mambo ya kufikiri au kubuni.

Aliyataja mengine yaliyoangaliwa na kuchambuliwa na jopo la wasomi kuwa ni namna taifa litakavyosimamia elimu yake kwa ufanisi katika ngazi za chini, wilaya mikoa na Taifa.

”Jambo jingine lililoangaliwa kisera ni namna tutakavyoiweka mitaala ya elimu iweze kutufikisha kwenye malengo ambayo ifikapo mwaka 2025 Tanzania itakuwa ni taifa lililosheheni watu

wa kipato cha kati ambacho kina wananchi wanaofahamu, wenye elimu, ujuzi, uwezo wa kupambanua na kuzikabili changamoto za maisha na ajira,” alisema.

Hata hivyo, Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, Isack Amani, akizungumza kwenye mahafali ya saba ya chuo hicho, alisema sekta ya elimu inahitaji mabadiliko makubwa kwa kuwa baadhi ya wasomi na wanafunzi hivi sasa wengi wao hawamudu kutekeleza majukumu yao kutokana na kutegemea akili zao zisukumwe na nguvu ya kilevi.

Chuo Kikuu cha Mwenge kimepandishwa hadhi kuwa Chuo Kikuu baada ya kujiengua katika mwavuli wa vyuo vingine 12 vishiriki vya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT)

CHANZO chingaone.com