Tuesday, November 18, 2014

Sikinde, Khadija Kopa jukwaani Nov.29

NA MWANDISHI WETU
MALKIA wa mipasho Tanzania, Khadija Kopa  na Bendi ya Sikinde ‘Ngpma ya Ukae’ wanatarajia kupanda kwenye jukwaa moja katika tamasha la sanaa na ubunifu la Mswahili maarufu kama Swahili Arts & Creative Carnival 2014, litakalofanyika Novemba 29 mwaka huu, kwenye Viwanja vya Posta Kinjitonyama jijini Dar es Salaam. 
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mratibu wa tamasha hilo, Ahadi Kakore amesema kuwa wameongeza bendi hiyo pamoja na Khadija Kopa kutokana na uwezo wao katika kazi na pia wamefanikiwa kuupeleka muziki wa Tanzania mbele.
“Maandalizi yanakwenda vizuri kwa sehemu kubwa hivyo niwaambie wapenzi wa burudani kwamba tamasha lao kwa ajili yao limeshawafikia.
“Pamoja na uwepo wa burudani ya muziki lakini  burudani nyingine zitakazopamba ni ni maonyesho ya filamu za Kiswahili, vyakula, maonyesho ya mavazi, nyama choma, vinywaji pamoja na michezo ya watoto huku tamasha likitarajiwa kuanza saa 5:00 asubuhi hadi usiku wa manane na watu 500 wa kwanza watapata zawadi langoni,” alisema Kakore.
Tamasha hilo limeandaliwa na Kampuni ya Swahili Arts & Creative Carnival kwa kushirikiana na Hildelly Solution na Wazalendo Bright Media kwa udhamini wa Amo Transport Solutions, Coca Cola, Tigo, Oriflem, Chibuku, Global Publishers, CTN na Sibuka TV.

No comments:

Post a Comment