Serikali
imesema wakati wowote kuanzia sasa, itaifuta sera ya elimu inayotumika
nchini kutokana na kukamilika kwa mchakato wa uanzishwaji sera mpya
ambayo imepangwa kuzinduliwa na Rais Jakaya Kikwete, mwezi huu.
Katibu Mkuu
wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome, alisema
sera hiyo tayari imepitishwa baada ya kujadiliwa na vikao vya Baraza la
Mawaziri.
Akizungumza
jana katika uzinduzi wa Chuo Kikuu kipya cha Mwenge (MWECAU)
kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki kilichopo nje kidogo ya mji wa Moshi,
Profesa Mchome alisema uamuzi huo wa Wizara hiyo umelenga kuhakikisha
kwamba sekta hiyo inakua na kukidhi mahitaji na matarajio ya jamii ndani
na nje ya nchi.
“Tumeanza
kuboresha elimu yetu kwa kuangalia eneo la mifumo ya kisera na kimsingi,
tumefumua sera inayotumika. Huko tumeangalia mwelekeo wa sasa wa dunia
inavyokwenda, mabadiliko ya sayansi na teknolojia, viwango na vigezo vya
ubora wa elimu inayotolewa,” alisema.
Alisema
mambo mengine yaliyohakikiwa wakati wa uandaaji wa sera mpya ni njia za
kuwapata wahitimu wenye elimu bora na yenye viwango ambavyo
vimebainishwa na kuwekwa kisera ili kuepusha mambo ya kufikiri au
kubuni.
Aliyataja
mengine yaliyoangaliwa na kuchambuliwa na jopo la wasomi kuwa ni namna
taifa litakavyosimamia elimu yake kwa ufanisi katika ngazi za chini,
wilaya mikoa na Taifa.
”Jambo
jingine lililoangaliwa kisera ni namna tutakavyoiweka mitaala ya elimu
iweze kutufikisha kwenye malengo ambayo ifikapo mwaka 2025 Tanzania
itakuwa ni taifa lililosheheni watu
wa kipato
cha kati ambacho kina wananchi wanaofahamu, wenye elimu, ujuzi, uwezo wa
kupambanua na kuzikabili changamoto za maisha na ajira,” alisema.
Hata hivyo,
Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, Isack Amani, akizungumza kwenye
mahafali ya saba ya chuo hicho, alisema sekta ya elimu inahitaji
mabadiliko makubwa kwa kuwa baadhi ya wasomi na wanafunzi hivi sasa
wengi wao hawamudu kutekeleza majukumu yao kutokana na kutegemea akili
zao zisukumwe na nguvu ya kilevi.
CHANZO chingaone.com
No comments:
Post a Comment