NA MWANDISHI WETU
BENDI Kongwe ya muziki wa dansi, Sikinde pamoja na Malkia wa
muziki wa Taarab Afrika Mashariki, Khadija Kopa ni miongoni mwa wanamuziki
watakatoa burudani kwenye Tamasha la Sanaa na Ubunifu wa Mswahili (Swahili Arts
and Creative Carnival).
Akizungumza na mtandao wa jamii, mmoja wa waratibu wa tamasha hilo, Ahadi
Kakore amesema kuwa Sikinde ni miongoni mwa bendi zinazopiga muziki wa
Kiswahili asilia ndiyo maana wameamua kuiweka kuwa bendi rasmi ya dansi ya
tamasha hilo.
Aliongeza kuwa kwa upande wa Khadija Kopa naye atakuwa na
bendi yake ya Ogopa Kopa Classic ambayo siku hiyo imeahidi kuimba nyimbo zake
mpya ambazo nyingi zitaimbwa kwa mara ya kwanza siku hiyo.
“Mbali ya kuwepo kwa burudani hizo za muziki lakini haina
maana kuwa ndiyo tumefunga mlango kwamba hatutakuwa na wasanii wengine ila bado
tupo kwenye mazungumzo na wanamuziki nyota wa kizazi kipya kwani tumelenga
kuwafikia watu wa rika zote.
“Pamoja na burudani za watu wazima pia watoto nao hawajaachwa
nyuma kwa sababu kutakuwa na michezo maalum kwa watoto na zawadi nyingi zipo
kwa ajili yao ili kuhakikisha wanafurahia siku hiyo.
Mbali na muziki, burudani nyingine zitakazokuwepo siku hiyo ni
maonyesho ya filamu za Kiswahili, maonyesho ya mavazi, vyakula, nyama choma,
vinywaji pamoja na michezo ya watoto na maonyesho ya bidhaa za wajasiriamali na
watu 1,000 wa kwanza watapata zawadi langoni,” alisema Kakore.
Swahili Arts and Creative Carnival linatarajiwa litafanyika
Novemba 29 mwaka huu kwenye viwanja vya Posta, Kijitonyama jijini Dar es Salaam
huku likiwalenga watu wazima na watoto kuanzia saa 4:00 asubihi hadi usiku wa
manane.
Tamasha hilo limeandaliwa na Kampuni ya Swahili Arts &
Creative Carnival kwa kushirikiana na Hildelly Solution na Wazalendo Bright
Media kwa udhamini wa Amo Transport Solutions, Coca Cola, Tigo, Oriflem,
Chibuku, Global Publishers, CTN na Sibuka TV.
No comments:
Post a Comment