MWIMBAJI wa nyimbo za injili na mcheza filamu za
Bongo, Martha Nelson, ni moja ya waimbaji wa muziki huo ambao wanafanya vizuri
katika tasnia hiyo kwa sasa.
Martha mama wa watoto watatu, licha ya kufanya
vizuri Afrika Mashariki kwenye muziki wa injili, lakini amekuwa akipata nafasi
za kuitangaza nchi katika maeneo mengine nje ya Afrika ikiwemo Ulaya na
Marekani.
Mwanamama huyu anasema kwamba, muziki wa injili
umekuwa ni kimbilio na kielelezo cha kumfanya atambulike kuwa ni Mtanzania
popote anapokuwa anakwenda, hasa kwa sababu kazi zake zote amekuwa akitumia
lugha ya Kiswahili.
Martha anasema ili kufanikiwa kwenye muziki wa injili lazima ufuate miiko inayoongoza muziki huo
nayo ni ukweli pamoja na kumshirikisha Mungu. Lakini lingine kuhakikisha kazi
inayofanyika ni bora ambayo inaweza kukubalika ndani na nje Tanzania.
“Kazi ya muziki wa injili ni ngumu lakini
ukimtegemea Mungu ni jambo linalowezekana kufanikiwa. Lakini kubwa kuliko yote
ni kujua unatakiwa kufanya nini kwa ajili ya nani.
“Kwa mfano katika kazi yangu mpya iitwayo ‘Yupo
Mungu Asiyeshindwa’ niliweza kumshirikisha Mungu kwa kiwango kikubwa naamini
ndiyo sababu ya kazi hiyo kufanya vizuri kwa wakati huu.
“Naelewa kuwa si jambo rahisi lakini niseme kwamba muziki
huu bado unahitaji nguvu ya ziada kuhakikisha unakuwa na kupaa zaidi ya ilivyo
sasa kwa sababu inawezekana kwani tunayemtumikia ni mkuu zaidi ya yeyote,”
anasema Martha.
Mwimbaji huyo anasema katika kazi hiyo mpya ina
jumla ya nyimbo nane ambapo kwa sasa imeshatoka ingawa sokoni itaingia katikati
ya Februari. Baadhi ya nyimbo zilizozopo kwenye albamu hiyo ni pamoja na
Usifiwe Jehova, Amenitoa Mbali, Acheni Niimbe na nyingine nyingi.
“Kazi hii natarajia itaingia sokoni katikati ya
Februari ili mashabiki wangu waweze kuniunga mkono, ingawa kubwa kuliko yote ni
kuhakikisha ujumbe wangu wa Neno la Mungu unawafikia watu wote.
Hii ni albamu ya pili kwa Martha ambapo ya kwanza
aliitoa miaka mitano iliyopita iliyokwenda kwa jina la Unawaza Nini.
“Baada ya kutoa albamu yangu ya kwanza nilikaa zaidi
ya miaka miwili nikiandaa kazi mpya, lakini baadaye nilikaa tena miaka hadi
kuingia studio na kurekodi video. Kwa lugha rahisi ni kwamba, kazi hii
nimeifanya kwa muda wa miaka mitano.
“Sababu kubwa zilizonifanya kuamua kuchukua muda
mrefu katika kazi moja ni kutokana na kutafuta ubora, unapotaka kufanya kitu
bora lazima ufanye kwa umakini lakini kitu chenye uhakika, mimi nilifanya hivyo
kwa kuamini kwamba ninaweza kufanya kitu bora hasa ikizingatiwa kuwa hii ni
kazi ya Mungu lazima iwe bora,” alisisitiza nyota huyo.
Mbali na kufanya vizuri kwenye muziki, lakini katika
tasnia ya filamu amefanya kazi nyingi ikiwemo Poster Shadow, Haki, Tutafika
pamoja na nyingine nyingi. Juu ya sekta hiyo, Martha ameishauri Serikali
kuhakikisha kuwa inaisimamia sekta ya filamu vizuri pamoja na sanaa kwa ujumla
ili kuzalisha ajira nyingi zaidi.
“Tunahitaji sanaa iwe ni kazi rasmi ambayo inaweza
kusimamia maendeleo ya uchumi kikamilifu. Naamini kuwa kwa kutumia njia hii itasaidia
katika mapambano dhidi ya umasikini,” amesisitiza mkali huyo wa injili.
Martha Nelson katika picha mbalimbali.