NA EZEKIEL TENDWA
LIGI Kuu ya England inatarajiwa
kuanza rasmi mwishoni mwa wiki ijayo ambapo nyasi za viwanja mbalimbali
zitawaka moto kila timu ikihitaji kujikusanyia pointi za mapema mapema kabla ligi
yenye haijachanganya.
Timu zote zimekuwa zikifanya
maandalizi ya nguvu kwa ajili ya kuhakikisha wanafanya vizuri wengine wakitaka
kuchukua ubingwa na wengine kuepuka mkasi wa kushuka daraja kwani katika soka
kila mmoja ana malengo yake.
Katika ratiba iliyotolewa na chama
cha soka nchini humo FA, inaonekana kuwabeba Manchester United katika michezo
yao sita ambapo kama wataingia na moto waliouonyesha nchini Marekani kwenye mechi
za kujiandaa na ligi hiyo, ambapo kama mwendo utakuwa huo huo watajikuta
wakikusanya pointi 18 za mapema bila kikwazo chochote.
Wakiwa nchini Marekani mabingwa
hao wa zamani wa England waliwatoa nishai
vigogo kama Los Angeles Galaxya Marekani, AS Roma na Inta Milan zote
zinazoshiriki Ligi Kuu ya Italia, Real Madrid ya Hispania pamoja na Liverpool
ya England.
Kikosi hicho ambacho kipo chini ya
kocha wao mpya Louis Van Gaal kitaanza mchezo wao wa kwanza Jumamosi ya wiki
ijayo dhidi ya Swansea, licha ya wapinzani wao kuwa katika kiwango kizuri
lakini uwezo wa kutoa upinzani kwa Mashetani Wekundu hao ni mdogo ingawa kwenye soka lolote
linaweza kutokea.
Mchezo wa pili kwa Van Gaal na
kikosi chake itakuwa dhidi ya Sunderland uwanja wa ugenini ambapo katika msimu
uliopita Sunderland licha ya kuwatoa kijasho Man United lakini historia inaweza
ikaendelea kuwabeba Man United.
Agosti 30 Man United, watakuwa
tena ugenini kukipiga na Burnley FC ukiwa mchezo wa tatu ambapo kutokana na ari
ya ushindi waliyonayo watataka kuondoka na pointi ili tu kujiwekea mazingira
mazuri ya kuhakikisha wanatafuta nafasi ya kushiriki michuano ya UEFA.
Wakati Arsenal wakiwa na kibarua
cha kuwakabili mabingwa watetezi wa michuano hiyo Manchester City katika uwanja
wao wa Emirates Septemba 13, kwa upande wao Man United wataendelea kujitafutia
pointi nyingine katika uwanja wao wa Old Trafford dhidi ya QPR Septemba 14.
Van Gaal atakuwa tena na kibarua
cha kutafuta pointi kwa timu ndogo ya Leicester ugenini Septemba 20 kabla ya
kumalizia kubarua cha kucheza na dhidi ya West Ham Septemba 27 kwenye uwanja
huo huo wa jijini Manchester.
Hiyo ndiyo michezo sita ambayo kwa
vyovyote Manchester United watatakiwa kutafuta pointi 18 kabla ya kuanza
kukwaana na vigogo ambapo baada ya michezo hiyo watavaana na wabishi Everton
kabla ya kupata mteremko mwingine dhidi ya West Bromwich Albion na baadaye kuja
kucheza na Chelsea 0ktoba 26.
Arsenal wao wataanza kwa mteremko
kidogo mchezo wa kwanza watakapocheza na Crystal Palace na baadae kukutana na
wabishi Everton ugenini huku Manchester City wao wakianza na wagumu Newcastle
kabla ya kuwavaa Liverpool.
Timu hizi kubwa za Manchester
United, Manchester City, Liverpool, Arsenal, pamoja na Chelsea ndizo
zinazotafuta nafasi nne za kwanza ili kupata tiketi ya kushiriki UEFA ambapo
msimu huu Manchester United wamepigwa kumbo baada ya kumaliza wakiwa nafasi ya
saba msimu uliopita.
Kwa maana hiyo ni kwamba msimu
ujao Ligi Kuu England itakuwa moto wa kuotea mbali kwani timu hizi vigogo moja
lazima iwapishe wenzake kwani sheria inaruhusu timu nne tu kutinga kwenye
michuano hiyo ya UEFA inayoheshimika duniani kote.
No comments:
Post a Comment