Wednesday, May 20, 2015

Tatizo la Stars ni kubwa zaidi ya tulionavyo

TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, inaendelea kufanya vibaya katika michuano mbalimbali, ikiwemo ya mashindano na ile ya kirafiki ambayo kimsingi ndiyo nguzo muhimu kwa timu hiyo kukua na kuendelea.
Nimekuwa mmoja wa watu waliokuwa karibu na Taifa Stars kwa misingi kwamba naifuatilia katika michuano yake mbalimbali, iwe ya nje au ile inayochezwa kwenye ardhi ya Tanzania.
Ninachokiona kwangu ni kitu kimoja kwamba kikosi cha Stars kina matatizo mengi, hasa ya uteuzi wa timu yenyewe ambayo kimsingi kimekuwa kiini cha matatizo ya timu hii ambayo ndiyo roho na kioo cha nchi katika sura ya kimataifa.
Tangi enzi za Kocha wa zamani wa timu hiyo, Marcio Maximo, kikosi hiki kimekuwa kina matatizo ya uteuzi na Watanzania wamekuwa wakijiuliza ni sifa gani ambazo zilikuwa zikitumika katika kuteua kikosi hicho.
Miongoni mwa wachezaji ambao watu walijiuliza kwa nini hawaitwi wakati walikuwa na uwezo ni kipa Juma Kaseja, ambaye alicheza muda mfupi sana akiwa na kikosi cha Stars, lakini mbadala wake alikuwa ni Ivo Mapunda.
Hata hivyo, ilipotokea Mapunda hayupo, aliyekuwa anapewa jukumu la kukaa langoni alikuwa ni Ally Mustafa ‘Barthez’, ingawa kwa wakati huo hakuwa akipata nafasi kwenye kikosi cha Simba alichokuwa akikitumikia.
Lakini baada ya kumalizika kwa utawala wa Maximo kwa muda wa miaka minne bila kombe lolote,  aliyekuja kuchukua nafasi yake, Jan Poulsen, aliwaita wachezaji wote kadri ilivyowezekana, hali ambayo iliweza kumsaidia kupata ubingwa wa Chalenji mwaka 2010.
Lakini baada ya hapo hatukuweza kushiriki fainali zozote kubwa, lakini wengi wa Watanzania pamoja na mimi niliamini kuwa kuna uwezekano wa kupatikana kwa matumaini kwa siku zijazo kama nchi, kwa maana kupata nafasi ya kushiriki japo michuano ya Afrika, yaani Afcon au ile ya wachezaji wa ndani, maarufu kama Chan, pia hilo tulilishindwa.
Ila kwa sababu wakati wa Babu Poulsen kulikuwa na mipango mizuri ya kuendeleza soka la vijana ambapo kulikuwa na msaidizi wake ambaye alikuja kuwa kocha mkuu, Kim Poulsen, wakati wa muunganiko huu tuliona mabadiliko makubwa kwenye timu ya taifa, ambapo zaidi walikuwa wakitumika vijana na timu ilikuwa na damu mchanganyiko.
Hii ilikuwa ni hatua moja mbele, lakini baada ya kuondoka kwa Jan pamoja na Kim, tunaanza kurudi kule kule kwamba timu ikaanza kupoteza hamasa kwa mashabiki na kuitwa kwa kikosi kukawa na ukakasi ambao hadi sasa umeendelea kuwepo, jambo ambalo kimsingi linafanya kurudi nyuma badala ya kwenda mbele kama zilivyo nchi nyingine.
Kwa mfano, katika kikosi cha mwaka huu ambacho kimekwenda kwenye michuano ya nchi za Kusini mwa Afrika, yaani Cosafa, kimelalamikiwa na kuwa na lawama nyingi kwa dawati la ufundi lililopo chini ya Kocha Mart Nooij, kwa kuachwa kwa baadhi ya wachezaji wenye uwezo na kuitwa wale ambao kimsingi hata katika ligi hawachezi au hawapo katika kikosi cha kwanza.
Kwa mfano, mchezaji kiungo kama Amri Kiemba ambaye kwenye kikosi cha Azam FC hana namba  kwenye kikosi cha kwanza, lakini ameitwa huku ligi amekuwa hachezi mara kwa mara. Hali hii ipo sawa na John Bocco, ambaye pamoja na kuwa nahodha, lakini hayupo kwenye kikosi cha kwanza cha Azam FC.
Kwa upande wa makipa, Mwadini Ally na Deo Munishi ‘Dida’ wanaitwa, lakini wapo wachezaji waliofanya vizuri zaidi ikilinganishwa na wachezaji hao tena kwa kucheza mechi nyingi.
Kwa mfano Barthez anaacha kuitwa wakati yeye ndiye kipa namba moja kwenye kikosi cha Yanga, hapa ndipo ninapoona tatizo la Stars ni kubwa kuliko linavyotazamwa, kwani inawezekana kabisa  Nooij, wasaidizi wake hawamsaidii kama inavyotakiwa, ndiyo maana amekuwa akiita wachezaji wasiostahili na kuacha wale wenye sifa.
Iinakuwaje leo hii unamuita Bocco mwenye mabao matatu kwenye ligi, lakini Rashid Mandawa mwenye mabao 10, Balimi Busungu mwenye mabao 8 wote wanaachwa? Naamini hapa kuna tatizo ambalo lazima kama nchi tuweze kulitatua haraka kwa manufaa ya nchi.
Ndiyo maana nimi nasisitiza kwamba katika suala la uteuzi wa wachezaji wa Stars, hasa msimu huu kumekuwa na matatizo makubwa ambayo hatutakiwi kuyafumbia macho, lazima tuambiane ukweli kama tunahitaji maendeleo ya kweli na nchi iweze kuendelea mbele, kwani sisi Watanzania ndiyo wenye mali.
Mimi niliamini kwamba ujio wa Mart Nooij huenda matatizo ya zaidi ya miaka sita yaliyokuwepo kwenye kikosi cha Stars yangekwisha, lakini imekuwa ni tofauti, kwani yameendelea kuwepo jambo ambalo naanza kupata shaka kuwa huenda makocha hawa wanaokuja kufanya kazi kwenye timu za taifa wanapewa uhuru kupita kiasi.
Uhuru huu ndio wakati mwingine unasababisha kuwepo kwa maamuzi ambayo si sahihi na hayana tija kwenye soka la Tanzania na timu yetu ya taifa kwa ujumla wake, kwani mafanikio tunayohitaji hatuyaoni.
Nadhani kuna sababu sasa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) kuchukua maamuzi magumu na kwamba Mkurugenzi wa Ufundi wa shirikisho hilo lazima awe mkali na kumweleza kocha nini ambacho Watanzania wanakihitaji.
Kwa kumbukumbu zangu ni kwamba, Stars chini ya Nooij imeweza kushinda mechi tatu tu kati ya mechi 14. Mechi ilizoshinda ni dhidi ya Zimbabwe bao 1-0 (kufuzu), dhidi ya Malawi bao 1-0 (kirafiki) na dhidi ya Benin mabao 4-1 (kirafiki), hapa ndipo ninapoona matatizo yanaendelea yale yale ya miaka yote ambayo bado hayajashughulikiwa.
Nilishangaa Kocha Nooij akisema kuwa amewaona wachezaji wote kwenye michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, hili inawezekana ni sawa, mbona wale bora waliofanya vizuri kwenye ligi hatujawaona kwenye kikosi cha Stars? Nadhani haya ni maswali magumu ambayo dawati la ufundi linafaa kuwaambia Watanzania. Lakini mwisho ni kwamba, tatizo la Stars ni kubwa zaidi ya tulionavyo.

IMEANDALIWA NA AHADI KAKORE KUTOKA KWENYE MAKALA YA USEMAVYO UBONGO WA KAKORE.

No comments:

Post a Comment