Tuesday, July 8, 2014

Ni vita ya kizazi cha dhahabu dhidi ya Messi leo

LEO kuna mchezo wa Kombe la Dunia hatua ya Nusu Fainali. Argentina wanaotoka Amerika ya Kusini, itapambana na Uholanzi inayotokea Ulaya, mchezo unaoonekana ni wa kisasi.

Kwa mtazamo wangu na jinsi nilivyoona, timu zote katika mechi zilizopita za hatua ya makundi, 16 bora, robo  hadi nusu fainali, naamini kwamba atakayeweza kupata ushindi katika mchezo wa leo ndiye atatwaa ubingwa.

Lakini mchezo wa leo nauangalia kwa darubini kali na kugundua kwamba Uholanzi ndio wenye nafasi kubwa ya kupita hata kutwaa ubingwa, kutokana na uwezo wao na historia ya timu hizo mbili zinapokutana kwa muda wa miaka 40 hivi sasa.
Historia inasema kwamba Juni 26 mwaka 1974 katika fainali za Kombe la Dunia mwaka huo, Uholanzi iliilaza Argentina mabao 4–0, huku mabao yakifungwa na Cruijff Goal katika dakika za 11 na 90, wakati mengine yakipachikwa na Krol Goal dakika ya 25, naye Rep Goal akimaliza karamu hiyo kufunga bao dakika ya 73.  

Lakini miaka 24 baadaye kwenye Fainali za Kombe la Dunia ya mwaka 1998, hatua ya Robo Fainali, mchezo uliopigwa Julai 4 mwaka 1998, Uholanzi iliibuka mbabe kwa mabao 2-1.

Kati ya mabao hayo mawili, moja lilifungwa na Patrick Kluvet katika dakika ya 12 na ikumbukwe kuwa nyota huyu yupo kwenye fainali hizi akiwa kwenye dawati la ufundi la timu ya Uholanzi, hivyo inaweza kuwa kichocheo kikubwa kwa timu hiyo kushinda.

Kadhalika timu hizi pia zilikutana kwenye Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Ujerumani ambapo zilipambana katika hatua ya makundi na kutoka sare ya bila kufungana mnamo Juni, 21 mwaka 2006.

Kwa historia hii napata uthubutu kusema kwamba, Uholanzi ndio wenye nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa msimu huu, hasa baada ya kufanikiwa kupita leo dhidi ya Argentina ambayo naiona imekuwa ni timu ya mchezaji mmoja au awaili tu. Wachezaji ambao Argentina inawategemea ni Lionel Messi anayecheza Barcelona ya Hispania pamoja na Angel di Maria ambaye leo hatakuwepo.

Kwa ufupi ni kwamba tangu mwaka 1934 katika fainali za kwanza za Kombe la Dunia, Uholanzi na Argentina zimekutana mara nne ambapo kati ya hizi, michezo miwili Argentina ilifungwa huku yenyewe ikishinda mechi moja na moja ikiwa ni sare ya bila kufungana.

Kwa lugha nyingine ninaweza kusema kwamba huu unaweza ukawa mwaka mzuri kwa Uholanzi, ambayo msimu uliopita ilikosa ubingwa mbele ya Hispania ambayo ilikutana nayo katika mechi yake ya kwanza nchini Brazil na kufanikiwa kuifunga mabao 5-1.

Lakini nikiangalia Argentina ya sasa ya Messi ni wazi kuwa haina uwezo wa kupambana na kikosi cha nyota kama Nahodha Robin van Persie, Wesley Sneijder au Arjen Robben, kikosi ambacho kinaundwa na wachezaji waliopo kwenye kiwango bora duniani kwa sasa.

Soka si mchezo wa kuweka dhamana kwa maana kwamba maajabu yanaweza kutokea,  kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa nusu fainali ya kombe hilo baina ya Brazil dhidi ya Ujerumani, kwani kulikuwa na pande mbili, moja ikiamini Ujerumani itashinda na nyingine Brazil itashinda, ila sasa ubishi umekwisha.

Hivyo kwa itakavyokuwa, mimi karata yangu ipo kwa Wadachi ambao wakivuka hapa ubingwa utakwenda kwa mara ya kwanza, kwani imekuwa na bahati mbaya ya kutotwaa kombe hilo, licha ya kufikia hatua za juu za mafanikio, ikiwemo fainali mara tatu ambazo ni mwaka 1974 dhidi ya Ujerumani Magharibi, 1978 dhidi ya Argentina na 2010 mbele ya Hispania.

Lakini yote tusubiri baada ya dakika 90 au 120 kumalizika na kuishuhudia Uholanzi ikielekea fainali na kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza, huku ikiwa na kizazi ambacho mimi nadiriki kukiita ni kizazi za dhahabu.

No comments:

Post a Comment