Tuesday, July 8, 2014

JURGE LOUIS PINTO



KOCHA Jurge Louis ambaye anaifundisha timu ya Taifa ya Costa Rica amejipatia umaarufu mkubwa baada ya kuifikisha timu hiyo katika hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Dunia zinazofanyika nchini Brazil.
Costa Rica ilitolewa na Uholanzi kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 4-3 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Fonte Nova, Jijini Salvador.

Timu hizo zililazimika kucheza dakika 120 baada ya kushindwa kufungana katika dakika 90 za kawaida na 30 za nyongeza na hatimaye Uholanzi kupita kwa mikwaju ya penalti, huku kipa wao aliyeingia dakika za mwishoTim Krul akiibuka shujaa baada ya kuokoa penalti mbili kati ya tano.

Costa Rica inasifika kuwa na mabeki imara ingawa pia ina washambuliaji bora kama vile Joel Campbell wa Arsenal, Bryan Ruiz na Tejeda ambao kwa pamoja huwa wanafanya kazi kwa pamoja.

Costa Rica ilifanya maajabu na kuwashangaza wengi katika michuano hii, kwani rekodi inaonyesha katika michezo iliyopita kabla ya Jumamosi hiyo ilikuwa imeruhusu nyavu zake kuguswa mara mbili tu, licha ya kucheza na timu ngumu ikiwemo Uruguay, Italia na England.

Baada ya mchezo huo wa Robo Fainali dhidi ya Uholanzi ambapo walitolewa mabao 4-3 yaliyopatikana kwa mikwaju ya penalti Kocha,  Jorge Luis alikaririwa na Shirika la Habari Reuters akisema kuwa licha ya  kufungwa, lakini timu yake imecheza vizuri.

“Katika michuano ya fainali ya Kombe la Dunia za mwaka huu, Costa Rica imefanya vizuri na kuwashangaza wengi ambao hawakuamini timu hii ingeweza kufika Robo Fainali.

“Costa Rica tulicheza na miamba ya soka duniani na tuliyaanga mashindano bila ya kufungwa, kwa kweli tuliwashangaza wengi na hii ni kutokana na timu kuundwa na wachezaji chipukizi, wenye vipaji,” anasistiza Kocha huyo.

Costa Rica katika michuano ya fainali za Kombe la dunia za mwaka huo kwanza ilizifunga Uruguay, Italia na kutoka sare na England na kuingia katika katua ya 16 bora. hatua ya mtoano ambayo ni mara ya pili katika historia ya timu hiyo.

“Timu ya Costa Rica ni miongoni mwa timu imara duniani pamoja na kwamba Kimataifa haiangaliwi kama timu nzuri, lakini baada ya kucheza michuano ya Kombe la Dunia tumethibitisha kuwa tupo katika ngazi moja na wao.

“Timu zote tulizocheza nazo katika michuano ya Kombe la dunia za mwaka huu zina wachezaji ambao wanacheza michuano ya Kombe la Ulaya, waliowahi kucheza katika fainali za Kombe la dunia michuano iliyopita na  ambao wanawakilisha timu zao katika ligi kubwa duniani.

“Kutokana na kiwango kizuri tulichoonyesha katika michuano hii nadhani tumeacha historia na kuwaoonyesha wapenzi kiwango cha soka cha Costa Rica kilivyo hivi sasa.

“Najivunia na hapo tulipofika, kwani tuliyaanga mashindano bila ya kufungwa katika dakika za kawaida pamoja na kwamba hatukuwa na bahati. Nakiri wachezaji wangu walishindwa kutumia vyema nafasi ya mikwaju ya penalti huku wapinzani wetu kutumia nafasi hizo vizuri ambazo ziliwawezesha kupata ushindi,” anasema Jorge Luis mwenye umri wa miaka 62.

Luis ambaye aliteuliwa kuinoa timu hiyo mwaka 2011, pia amewahi kuifundisha timu ya Taifa ya Colombia. Alizaliwa Desemba 16, 1952 katika Mji wa San Gil, Colombia.

Makala hii imetayarishwa na HENRY PAUL kwa msaada wa mashirika mbalimbali ya habari.

SALVADOR, Brazil

No comments:

Post a Comment