Naibu Waziri
wa Maji, Amos Makalla, jana aliondolewa chini ya ulinzi mkali wa polisi
katika mkutano wa hadhara baada ya kuzuka vurugu zilizotokana na
wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wa Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), jijini Dar es Salaam.
Vurugu hizo
zilizodumu kwa takriban dakika 30, zilitokana na Mwenyekiti wa CCM
Wilaya ya Kinondoni, Salum Madenge, kusalimia wananchi katika mkutano
huo, kitendo ambacho kilionekana kutowapendeza wafuasi wa Chadema kwa
madai kuwa haukuwa mkutano wa CCM.
Tukio hilo
lilitokea jana katika uwanja wa Goba, jijini Dar es Salaam, wakati
Makalla alipowasili na viongozi mbalimbali kutoka wizara hiyo pamoja na
viongozi wa CCM na Chadema kwa ajili ya kuzungumza na wananchi wa kata
hiyo kuhusiana na tatizo la maji na namna serikali ilivyojipanga kutatua
kero hiyo.
Kitendo cha
mwenyekiti huyo wa CCM kusimama na kusalimia wananchi hao, kiliwafanya
wafuasi wa Chadema kulipuka na kuanza kuvamia uwanja wakimtaka aondoke.
Wafuasi hao wa Chadema walisema mkutano haukuwa wa CCM na kwamba,
walichokuwa wakikitaka ni maji na siyo viongozi wa CCM kuzungumzia ilani
zao.
Kitendo
hicho kiliwafanya wafuasi wa CCM nao kuanza kupiga kelele za kuwataka
viongozi wa Chadema waliokuwa wamekaa jukwaa kuu kuondoka ili kuwapo na
usawa.
Kutokana na
kelele za wafuasi hao kukithiri, askari polisi waliokuwapo walilazimika
kutumia nguvu za ziada kuwadhibiti wafuasi hao.
Polisi waliwazingira viongozi waliokuwa jukwaa kuu kulinda usalama wao uliokuwa umetishiwa na wafuasi wa vyama hivyo.
Hata hivyo,
juhudi za polisi hazikufua dafu kwani vurugu ziliongezeka na hivyo
kuwalazimu kumuondoa jukwaani Makalla na kumuingiza kwenye gari lake,
huku viongozi wa Chadema wakiendelea kuzozana na polisi.
Akizungumza
na waandishi wa habari baada ya kuondolewa jukwaani akiwa ndani ya gari
lake, Makalla alisema vurugu hizo zimesababisha wananchi wakose haki yao
ya msingi kwa sababu siasa zimeingilia kati mkutano huo.
“Haya
niliyatarajia. Kwa hiyo, siwezi kushangaa wakati wananchi wengine wakiwa
wanafurahia ujio wa waziri katika maeneo yao watoe malalamiko yao, hali
imekuwa ya kisiasa zaidi na matokeo yake tumeshindwa kuzungumza na
wananchi mambo ya msingi,” alisema Makalla.
Alisema
amekamilisha jukumu lake kwa kufika kwa wananchi ili awaeleze mipango ya
serikali ya kutatua kero ya maji, lakini mkutano umeingiliwa na
wanasiasa wasio wakazi wa kata hiyo.
Kwa upande
wake, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, alisema vurugu hizo
zimetokana na wafuasi wa CCM, ambao siyo wakazi wa eneo hilo kuingilia
kati ili Makalla asizungumze na wananchi.
“Kitendo cha
Makalla kuondoka na kuacha wananchi wakiwa hapa, huku wanachama wake
wakiendelea kufanya vurugu ni wazi kuwa anakwepa kujibu maswali ya
wananchi kuhusu masuala ya maji. Hivyo, sisi hatutaondoka mpaka
wanachama wetu wafahamu ni lini watapata maji,” alisema Mnyika.
Awali,
Makalla na Mnyika walitembelea maeneo ya Kigogo na kuwakamata watuhumiwa
watano wa wizi wa maji, ambao walikuwa wamejiunganishia maji kinyemela.
Akizungumza
baada ya kufanya ukaguzi katika nyumba hizo, Makalla alisema viongozi na
wananchi wana majukumu ya kuwatambua na kuwaripoti watu, ambao
wanahujumu uchumi wa nchi.
Alisema watu watano waliokamatwa wanaikosesha Dawasco mapato aliyodai ni Sh. bilioni 1.2 kwa mwezi.
“Hawa, ambao
wamekamatwa leo, lazima wafikishwe katika vyombo vya dola ili
kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwamo kuwagawia wananchi maji yote
waliyoyahifadhi katika matanki yao, pamoja na mali zao kuwa chini ya
ulinzi wakati sheria inachukua mkondo wake,” alisema Makalla.
Makalla
alianza ziara juzi katika jiji la Dar es Salaam kukagua miundombinu ya
maji pamoja na kuzungumza na wananchi kuhusiana na kero za maji na namna
serikali ilivyojipanga kumaliza tatizo hilo.
HABARI NA MARY GEOFREY
CHANZO - NIPASHE
No comments:
Post a Comment