NI wazi kwamba Yanga sasa itakuwa tishio! Hilo limedhihirika jana baada ya klabu hiyo kumleta rasmi nchini straika Mbrazil mwingine, Ginilson Santos 'Jaja' kwa ajili ya kufanya majaribio na kama atafuzu, kibarua cha mmoja kati ya mastraika wawili wa timu hiyo kutoka nchini Uganda, Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza, kitakuwa kimeota mbawa.
Kama hiyo haitoshi, neema mpya imetua kwa wachezaji wake, baada ya Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kutangaza fursa za mikopo, zitakazowawezesha wachezaji wa timu hiyo kumiliki nyumba zao.
Mashabiki wa klabu hiyo waliokuwa wamekusanyika kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere jana walikumbwa na kiwewe baada ya kumshuhudia straika wao mpya Mbrazil, Jaja akiwasili nchini tayari kukipiga katika klabu yao ya Jangwani.
Jaja anakuwa mchezaji wa pili kutoka nchini Brazil baada ya mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Tanzania Bara kufanikiwa kunasa saini ya Andrey Coutinho, ambaye kwa sasa anaendelea kujifua na wachezaji wenzake.
Kwa maana hiyo ni kwamba mpaka sasa Yanga inao watu wanne kutoka nchini Brazil, wakiongozwa na Kocha wao Mkuu, Marcio Maximo, Kocha Msaidizi Leonado Neiva na wachezaji wawili, Andrey Coutinho na Jaja.
Jaja aliwasili nchini jana saa nane mchana na kupokelewa na mashabiki na baadhi ya viongozi, akiwamo Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto.
Baada ya kutua kwa Jaja jana, klabu hiyo sasa imefikisha idadi ya wachezaji sita wa kigeni ambao ni Hamis Kiiza, Haruna Niyonzima, Mbuyu Twitte, Emmanuel Okwi, Jaja pamoja na Coutinho.
Kwa maana hiyo ni kwamba Yanga watatakiwa kumtema mchezaji mmoja kati ya hao ili kubakiwa na wachezaji watano wa kigeni kama kanuni za Shirikisho la Soka nchini, TFF zinavyotaka.
Taarifa ambazo zipo zinadai kuwa kati ya wachezaji hao, Okwi na Kiiza mmoja kati yao ana hatihati ya kutemwa ili kuwapisha Wabrazil hao ambao wanatarajiwa kuonyesha makeke yao, hasa msimu ujao na michuano ya kimataifa inayowakabili.
Ijumaa iliyopita wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya mazoezi yaliyofanyika katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola, Kocha Mkuu wa Yanga, Maximo alikaririwa akisema timu yao itafanya usajili mzuri na wa kushtukiza.
Alisema lengo la kufanya usajili huo ni kuhakikisha Yanga inafikia malengo ya juu kama zilivyo timu kubwa za Afrika, akitolea mfano TP Mazembe ya Kongo wanakochezea Watanzania Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
Kuhusu wachezaji kukopeshwa nyumba, habari hiyo njema ilifikiwa katika kikao cha pamoja kati ya uongozi wa klabu hiyo na wenzao wa NSSF, kilichofanyika jana katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu, alisema wachezaji wake wataichangamkia fursa hiyo kwa vile uongozi wao ulikuwa na mikakati ya kuboresha maisha ya wachezaji wao.
Njovu alifafanua kwamba Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji, ndiye atakayekuwa mdhamini wa wachezaji na pia atasimamia urejeshwaji wa mikopo kwa kila mchezaji atakayeomba.
Katika mpango huo, mchezaji atalazimika kulipa Sh mil. 2.5 na kisha kukabidhiwa nyumba na baadaye atakatwa hadi zitakapokamilika Sh mil. 64 ambayo ndiyo thamani halisi ya nyumba hizo.
Naye Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Crecentius Magori, aliwataka wachezaji kujiunga na mfuko huo ili kupata bima itakayowasaidia kupata matibabu kwa gharama nafuu.
Alifafanua kwamba endapo mchezaji atachangia Sh 20,000 kwa mwezi, baada ya miezi mitatu ataanza kupata faida ya matibabu pamoja na huduma nyingine zinazotolewa na mfuko huo.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Kocha Mkuu wa Yanga, Marcio Maximo, ambaye ameufurahia mpango huo na kudai kwamba wachezaji watafanya vizuri kwa vile watakuwa na utulivu.
Beki kisiki wa Yanga, Mbuyu Twite, amekuwa wa kwanza kuonyesha nia ya kuchangamkia mkopo huo.
Twite alisema yeye ndiye atakayekuwa wa kwanza kujiunga miongoni mwa wachezaji wenzake ili ajipatie nyumba hiyo.
"Hapa Tanzania ni nyumbani, endapo nitapata nyumba itakuwa kama sawa nimejenga kwetu DRC," alisema.
Katika hatua nyingine, wachezaji wa Yanga wamejikuta katika wakati mgumu kutokana na dozi ya mazoezi waliyoongezewa na kocha wao, Maximo, aliyetua hivi karibuni kukinoa kikosi hicho.
Wakati anatua nchini, Maximo aliwaahidi mashabiki wa timu hiyo kwamba amekuja kuifanya Yanga kuwika kitaifa na kimataifa, ndiyo maana anataka kauli yake hiyo itimie.
Yanga wanafanya mazoezi yao katika uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola jijini Dar es Salaam kila siku asubuhi, wakitumia saa tatu chini ya kocha huyo ambaye alishawahi kuifundisha timu ya Taifa, Taifa Stars.
Katika mazoezi ya kocha huyo, anao utaratibu mmoja kwamba yule mchezaji anayeonekana hana pumzi ya kutosha huamriwa kukimbia, kuuzunguka uwanja mzima zaidi ya nusu saa, lengo likiwa kwenda sambamba na wenzake.
Hali hiyo iliwakumba baadhi ya wachezaji, akiwamo Mbrazil mwenzake, Andrey Coutinho, Said Bahanuzi, Salim Telela, Omega Seme na beki wa kulia, Mbuyu Twitte.
Akionekana kudhamiria kuimarisha safu yake ya ushambuliaji, Maximo jana alikuwa na kazi ya kuwafundisha namna ya kufunga mabao ambapo Jerryson Tegete, Nizar Khalfani pamoja na Coutinho walionekana kumudu vema zoezi hilo.
Kwa upande wa safu ya ulinzi, licha ya mabeki wake wa kati Kelvin Yondani na Nadir Haroub 'Cannavaro' kukosekana kutokana na kuwa katika kikosi cha Stars, hakuna kilichoharibika, kwani Mbuyu Twitte, Rajab Zahir, Juma Abdul pamoja na Abuu Ubwa wameonyesha ushirikiano mkubwa.
Kwa maana hiyo, kama Yondani na Cannavaro wakirejea kuungana na wenzao hao, hakika dawa ya mshambuliaji wa Simba, Amis Tambwe itakuwa imepatikana na hatawasumbua tena Yanga.
Imeandikwa na Saada Akida, Ezekiel Tendwa na Humphrey Shao.
No comments:
Post a Comment