Tuesday, October 28, 2014

Usemavyo ubongo wa Kakore




Hawa wametolewa kafara, tatizo lipo Simba
HIVI karibuni klabu ya Simba ilitangaza kuwasimamisha wachezaji wake watatu kwenye kikosi hicho ambao ni Haruna Chanongo, Shaaban Kisiga na Amri Kiemba kwa kile kilichoelezwa kuwa ni utovu wa nidhamu.
Lakini hapa najiuliza maswali mengi kuwa ni kweli tatizo la Simba ni Kiemba, Kisiga na Chanongo, Kocha Patrick Phiri na wasaidizi wake? Au kuna matatizo mengine makubwa zaidi ya haya tunayoyaona yakitokea sasa.
Lakini majibu ni mepesi ambayo hayahitaji hata elimu ya darasa la saba kujua ukweli wa mambo kwamba tatizo la Simba ni kubwa zaidi ya Kiemba na wenzake ambao mimi naamini kuwa wametolewa kafara huku matatizo ya msingi yakiachwa.
Ukiangalia Simba ilivyo sasa ina mpasuko na mgogoro uliotokana na makovu ya uchaguzi ambayo yalipelekea wanachama zaidi ya 60 kufukuzwa uanachama wao kwa kosa la kufungua kesi mahakamani wakati wa uchaguzi uliofanyika yapata siku 100 zilizopita.
Hii ni moja ya sababu kubwa ambayo inaifanya Simba ipepesuke kwenye ligi kwani ukweli uliopo ni kwamba kama klabu ikiwa haina umoja na amani ni ngumu kupata matokeo bora, jambo hili ndilo linaikumba Simba kwa sasa hivyo kuwaondoa kikosini wachezaji hawa ni tatizo lingine linaloendelea kutengenezwa katika timu badala ya kutatua.
Naamini kwamba, baada ya kuwafukuza au kuwaondoa kikosini Kiemba na wenzake, bado ndani ya timu hapawezi kuwa na utulivu kwani wapo wachezaji ambao wanaweza kucheza kwa hofu kwa kuamini kuwa nao wanaweza kufukuzwa jambo ambalo litawafanya kucheza chini ya kiwango.
Lakini jambo la pili ni kukosekana kwa mshikamano na sauti moja ambayo inaifanya Simba kuwa moja kama ambavyo kauli mbiu yake inavyosema ‘Nguvu Moja’, hii ni kutokana na mpasuko ambao niliueleza hapo awali.
Kwa maana hiyo ili kuwa na Simba imara, ni lazima kuhakikisha inawarejesha Wanasimba kwenye nyumba moja kwa njia ya kukusanya makundi yote na kuwa kwenye njia rahisi ya kuelekea kwenye mafanikio.
Juu ya jambo hili lazima uongozi wa Simba ukae na kufikiria namna bora ya kufanya ili Simba kuwa moja vinginevyo hayawezi kupatikana matokeo bora ndani ya timu hiyo kwa wakati huu. Nakumbuka nilishasema miezi kadhaa iliyopita kuwa suala la mpasuko na mgogoro ndani ya Simba linaweza kusababisha matatizo makubwa kwa wakati huo na wakati ujao ambao ndiyo haya tunayoyaona sasa.
Jambo la tatu ambalo ni miongoni mwa mambo nyeti ni ukosefu wa stamina kikosini, ambapo timu imekuwa ikichoka mapema ndiyo maana yenyewe imekuwa ikicheza muda wa dakika 45-60 pekee hivyo zinazobakia wapinzani wao wanakuwa wakimiliki mpira.
Kwa hali hiyo imefanya hata kama Simba inapata ushindi lakini inakwama kuulinda ushindi huo na matokeo yake kuruhusu mabao rahisi na wakati mwingine ni tofauti na jinsi ilivyopata mabao yake.
Haya ni mambo ambayo Simba inastahili kuyaangalia na kuyatolea maamuzi wakati huu kutokana na unyeti wake kwani tatizo la kiufundi linaonekana ingawa naamini linatokana na mambo nje ya dawati la ufundi.
Ninachokifahamu ni kwamba, iwapo Simba inahitaji matokeo bora ni lazima iangalie katika nyanja mbalimbali na si kuwafukuza wachezaji au kumfukuza kocha kwani naye taarifa zilizopo ni kwamba amepewa mechi tatu akishindwa kufanikiwa safari itakuwa imemkuta.
Ila naamini kocha akishafukuzwa wapo viongozi nao wanastahili kujiuzulu kwa manufaa ya klabu kwasababu kama wameshindwa kuongoza ni vizuri wakaachia Wanasimba wengine waweze kuongoza kwani huenda wakawa na mbinu mbadala za kuifanya Simba kupata ushindi.
Kwa mfano katika mchezo baina ya Simba na Caostal Union kwenye Uwanja wa Taifa, Simba ilitangulia kufunga lakini ikashindwa kuulinda ushindi wake na kujikuta inaambulia sare, mwenendo ambao umekuwa ukiendelea hivyo hivyo hadi sasa.
Ndiyo maana nasema kuwa tatizo la Simba si Kisiga, Chanongo wala Kiemba ila kuna matatizo mengine mengi ndani ya timu ambayo yameifanya Simba kushindwa kuwa bora ambapo moja ya sababu hizo ni kuwepo kwa mgawanyiko miongoni mwa wachezaji.
Kwa sasa ndani ya timu moja kuna wachezaji ambao wanaonekana ni bora na muhimu kuliko wengine, jambo hilo nalo linatajwa kuchangia Simba kushindwa kufanya vizuri hivyo lazima uongozi uchukue hatua ya kurekebisha matatizo hayo badala ya uamuzi wa huwatuhumu wachezaji hawa wanaijuhumu timu.
Kwa sasa Simba ipo katika nafasi ya 10 baada ya kucheza mechi tano, ikitoa sare mechi tano, ikifungwa mabao matano na ikiwa na pointi tano, lakini hadi sasa haijafungwa takwimu ambazo mimi naamini si mbaya ila nafasi iliyopo ndiyo mbaya ingawa kama matatizo niliyoyataja yakirekebishwa, inaweza kuisaidia timu hiyo kufanikiwa.
Mazingira ya sasa yanastahili kufanyiwa maamuzi ya busara ili kufanikiwa vinginevyo uongozi unaweza kuingia kwenye historia mbaya ya timu kushuka daraja ikiwa mikononi mwao jambo ambalo litakuwa ni la aibu ya mwaka ambayo haijaweza kumkuta kiongozi yeyote kwenye klabu hiyo kwa zaidi ya miaka 70.

No comments:

Post a Comment