JUMA KASESA NA EZEKIEL TENDWA
YANGA SC imeifanyia umafia Kagera Sugar kwa
kutanguliza kikosi kazi maalumu kwenda kuichunguza timu hiyo, kabla ya mchezo
wao na timu hiyo Jumamosi wiki hii kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Kikosi cha kocha Mbrazil Marcio Maximo kinataka
kuendeleza wimbi la ushindi ili kutimiza dhamira yao ya kutwaa ubingwa wa Ligi
Kuu unaoshikiliwa na Azam FC.
Kwa kutambua Kagera ni wagumu kufungika nyumbani,
Yanga imefanya tena kile ilichokifanya msimu uliopita kwa kutuma kikosi kazi
maalumu cha kuichunguza timu hiyo mbinu zake ili kurahisisha mipango yao ya
kuondoka na pointi tatu Uwanja wa Kaitaba.
Msimu uliopita Yanga ilituma jopo la matajiri
wakiongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, Stanley Katabaro
ambaye ana asili ya Mkoa wa Kagera na baadhi ya wajumbe wenzake wa Kamati ya
Utendaji kwenda kuichunguza timu hiyo na kuwasilisha taarifa muhimu kwa benchi
la ufundi wakati huo likiwa chini ya kocha Fred Felix Minziro 'Majeshi'.
Na safari hii Yanga imetuma jopo la watu maalumu wa
benchi la ufundi kwenda Wilaya ya Misenyi, ambako Kagera Sugar imejichimbia
ikijifua chini ya kocha wake, Jackson Mayanja tayari kwa mchezo huo ambao ni
gumzo kwa sasa.
Habari za uhakika kutoka ndani ya uongozi wa Yanga
zimelieleza DIMBA Jumatano kwamba, jopo hilo limeshaingia Misenyi
likiwachunguza wachezaji wa Kagera na limekuwa likiwasilisha taarifa kwa benchi
la ufundi kila inapomalizika programu ya mazoezi ya timu hiyo.
Aidha, imeelezwa kikosi kazi hicho kilichopelekwa si
rahisi kugundulika kwani Yanga imebaini ingempeleka tena Katabaro safari hii
ingeweza kushtukiwa mpango wake mapema na Kagera.
Itakumbukwa Yanga ilikuwa haijapata ushindi uwanja
huo tangu mwaka 2011 kabla ya kuvunja mwiko huo Oktoba 12, 2013 kwa kuichapa
Kagera Sugar mabao 2-1.
Shukrani kwa mabao ya Mrisho Ngassa dakika ya 2 na
Hamis Kiiza 'Diego' dk 60, yaliyoiwezesha timu hiyo kuondoka na ushindi kwenye
uwanja huo.
Kikosi cha Yanga kimejichimbia Kahama kabla ya
kuelekea Bukoba ambapo leo kinatarajiwa kucheza mchezo wa kujipima nguvu dhidi
ya Ambassador FC ya mjini humo.
Maximo ameupania mchezo huo na ndio maana ameamua
kusafiri na kikosi chake chote cha wachezaji 28 ambapo jana walijifua
kikamilifu kuhakikisha wanarudi Dar es Salaam na ushindi mnono kutoka kwa
wakata miwa hao wa Kagera.
Kikosi cha Maximo kitaingia kwenye mchezo huo kikiwa
na kumbukumbu nzuri ya ushindi mnono wa mabao 3-0 iliyoupata kwa Stand United
mwishoni mwa wiki iliyopita wakati Kagera wao watakuwa na hasira ya
kulazimishwa sare 1-1 nyumbani na 'Wagosi wa Kaya' Coastal Union.
Maximo amesema kwa sasa akili yake yote ni
kuhakikisha hadondoshi pointi hata moja iwe ni Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam au viwanja vya mikoani yote hayo ikiwa ni kutimiza ahadi ya kuipa Yanga
ubingwa.
Kocha huyo anajivunia kikosi kilichokamilika kila
idara kuanzia golini hadi safu ya ushambuliaji ambapo hayo yote
yalijidhihirisha katika mtanange dhidi ya Stand United walipopata ushindi mnono
wa mabao 3-0 ambayo tangu ligi ianze msimu huu hawajawahi kuyafunga.
Jeuri kubwa aliyonayo Maximo ni kurudi kwa kiwango
cha mshambuliaji wa timu hiyo, Jerryson Tegete alipofunga mabao mawili kwenye
ushindi huo dhidi ya Stand huku lingine likifungwa na Mbrazil Geilson Santos
‘Jaja’.
Kazi kubwa iliyopo kwa Maximo ambayo inamfanya akune
kichwa ni namna ya kuamua nani amuanzishe kikosi cha kwanza na nani abaki hasa
kwenye safu ya ushambuliaji huku viungo nao wakipigana vikumbo kwa kuonyesha
uwezo mkubwa.
Kutokana na kazi kubwa iliyoonyeshwa na Tegete kwa
kufunga mabao mawili ni dhahiri kazi itakuwa kubwa kwa Jaja kuhakikisha
anatetea nafasi yake hiyo ambapo pia Husein Javu pamoja na Nizar Khalfani nao
wanakuja juu.
Kwa sasa kwenye kikosi cha Yanga, Tegete ndiye
anayeongoza katika suala zima la upachikaji wa mabao mawili licha ya kwamba
amecheza kwa dakika chache katika mchezo mmoja dhidi ya Stand United huku
michezo yote minne akisugulishwa benchi.
Yanga wapo nafasi ya tatu wakiwa na pointi 10 sawa
na Azam FC iliyopo nafasi ya pili huku Mtibwa Sugar wakiwa kileleni baada ya
kujikusanyia pointi 13 timu zote zikiwa zimecheza mechi tano.
Kwa upande wao Kagera Sugar ambao watakuwa uwanja
wao wa nyumbani kuwakabili Yanga, wapo katika nafasi ya saba na pointi sita
ambapo mchezo wao huo unatabiriwa kuwa mkali kila timu ikihitaji kusogea mbele.
No comments:
Post a Comment