NA JIMMY CHIKA
KOCHA wa Simba Mzambia, Patrick Phiri amefumba macho
baada ya uongozi wa klabu hiyo kuwapiga chini nyota watatu wa timu hiyo,
akapiga ngumi kifuani na kusema kikosi chake sasa kitazaliwa upya.
Phiri amesema uamuzi huo umerudisha ari yake ya
kukinoa kikosi hicho kwani kabla ya hapo alionekana kukata tamaa.
Jana kocha huyo alikataa kufafanua juu ya tishio la
Kamati ya Utendaji ya Simba iliyoketi mkoani Iringa na kutoa maamuzi ya
kuwatimua wachezaji wake watatu, Shaaban Kisiga, Haruna Chonongo na Amri
Kiemba, lakini akasema mabadiliko yaliyofanyika anaamini yataleta taswira mpya.
Akizungumza na gazeti hili, Phiri alisema yeye kama
kocha aliwaambia viongozi wakae na kuangalia tatizo liko wapi na walirekebishe
kwa hiyo anaamini kama waliona tatizo liko kwa wachezaji hao basi wametekeleza maagizo yake.
Hata hivyo, mabadiliko hayo hayakupokewa vizuri na
mashabiki wa Simba ambapo jana baadhi yao walivamia makao ya klabu hiyo na
kuendesha vikao visivyo rasmi kupinga hatua hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mashabiki hao
walisema, kinachoigharimu Simba kwa sasa ni hali ya kutokuwepo kwa uhusiano mzuri
baina yao na kamwe si wachezaji.
Mashabiki hao wamewatetea wachezaji hao ambao wote
hucheza nafasi ya kiungo, kuwa watahitajika sana katika mechi zijazo hasa
kutokana na uzoefu wao.
Kiemba ambaye ndiye pekee aliyeongelea suala la
kutimuliwa kwao, alisisitiza kwamba amepoteza ari ya kuitumikia timu hiyo
kufuatia kitendo hicho alichokiita ni udhalilishaji kwake.
Rais wa klabu hiyo, Evance Aveva alitaja sababu ya
kutimuliwa Kiemba kuwa ni kushuka kiwango, huku Kisiga na Chonongo wakituhumiwa
kwa utovu wa nidhamu.
Hata hivyo, Aveva aliliambia DIMBA kwamba, wachezaji
hao bado wako chini ya klabu hiyo hadi pale kikao cha kuwajadili
kitakapofanyika keshokutwa Ijumaa na kutoa maamuzi ya pamoja.
Wakati hali ikiwa hivyo, uongozi wa Simba umempa
Phiri mechi mbili zijazo za kushinda, dhidi ya Mtibwa Sugar Jumamosi hii na
Ruvu Shooting wiki ijayo, vinginevyo utavunja mkataba wake.
Phiri amepewa mechi hizo ili kuinasua timu hiyo
kutoka dimbwi la sare ambalo limeiandama timu hiyo tangu kuanza kwa ligi.
Katibu Mkuu wa Simba, Stephen Ally aliwaambia
waandishi wa habari jana makao makuu ya klabu hiyo Mtaa wa Msimbazi kuwa, Phiri
anaweza kuondolewa baada ya mechi hizo mbili iwapo matokeo hayatakuwa mazuri.
Ally amesema kwamba, sababu ya Kamati ya Utendaji
kufikia maamuzi hayo ni kwamba, wakati anaajiriwa Agosti mwaka huu, Phiri
alipewa kila alichokihitaji ili kujenga timu.
"Alitaka kambi ya Zanzibar akapewa, akataka
mechi za majaribio akapatiwa na timu imeendelea kuwa kambini muda wote wa
mashindano, ikiwemo ya Afrika Kusini," alisema Ally.
Phiri alifanya vizuri katika mechi za kirafiki,
lakini baada ya kuanza kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzaia Bara ametoa sare mechi
zote tano na Jumamosi wiki hii atakuwa Uwanja wa Jamhuri dhidi ya vinara,
Mtibwa Sugar.
Aidha, Katibu huyo amesema kwamba wachezaji watatu
waliosimamishwa, Kisiga, Amri Kiemba na Haroun Chanongo watakutana na Kamati ya
Nidhamu Ijumaa kujibu tuhuma zao.
Katika hatua nyingine mechi ya Simba na Mtibwa
inazidi kuwa katika mazingira magumu kwa timu hiyo ya Msimbazi hasa
ikizingatiwa kwamba wachezaji wengine nao wamepewa sharti la kushinda mechi
hiyo ili kuepuka adhabu kama iliyowakumba wenzao.
Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao,
baadhi ya wachezaji wameelezea kuihofia mechi hiyo kuliko ilivyokuwa ile
iliyowakutanisha na Yanga, iliyopigwa Oktoba 18 kwenye Uwanja wa Taifa na
kumalizika kwa matokeo ya suluhu 0-0.
Kwa upande wao uongozi wa Mtibwa Sugar umewataka
wenzao wa Simba kutumia busara kumaliza matatizo yao lakini wasiuchukulie
mchezo wao kama kigezo cha kutimua wachezaji.
Kocha wa Mtibwa, Mecky Mexime aliliambia DIMBA
kwamba, maandalizi yao na nia ya kutwaa ubingwa msimu huu ndiyo iliyowafikisha
hapo na kwamba wana uhakika wa kushinda mechi yao dhidi ya Simba itakayopigwa
kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Emmanuel Okwi (jezi nyekundu), mmoja wa wachezaji tegeemo kwa kikosi cha Patrick Phiri.
No comments:
Post a Comment