TIMU ya soka ya Yanga imekumbana na hujuma za aina yake kutoka kwa wenyeji wao, Etoile du Sahel, waliokuwa nchini humo kwa ajili ya mchezo wao kwa lengo la kuwatoa kimchezo katika mechi yao wao ya marudiano ya Kombe la Shirikisho.
Lengo la Waarabu hao lilikuwa ni kuwatoa mchezoni, kwani imekuwa ni kawaida kwa timu za nchi hizo kulalamikiwa kwa kuzifanyia hujuma timu wanazocheza nazo katika viwanja vyao vya nyumbani ndani na nje ya uwanja, kitu ambacho kwa dunia ya sasa hakikubaliki.
Yanga walianza kukutana na vitimbi hivyo siku ya kwanza tu walipotua, baada ya kugandishwa uwanja wa ndege kwa saa mbili, huku wenyeji wao hao wakidai wanashughulikia suala la viza, lakini kumbe ilikuwa mbinu ya kuwachosha.
Baada ya kuona hivyo, Yanga, ambayo katika mchezo wa kwanza uliopigwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ililazimishwa sare ya bao 1-1, walikuja juu na kuanza kupiga kelele wakitaka kutendewa haki, ndipo wenyeji wao hao walipofanya jitihada za kushughulikia suala hilo.
Hata hivyo, Yanga walijua mchezo mchafu watakaochezewa na wenyeji wao, hivyo walijiandaa kifedha na kukodi gari zuri kubwa lililowabeba wachezaji na kuwa katika usalama zaidi, baada ya awali wenyeji wao kuwaletea basi lililokuwa bovu.
Mbali na hujuma hizo, Rais wa timu ya Etoile du Sahel na maofisa wa timu hiyo pamoja na benchi la ufundi, juzi walivamia mazoezi ya Yanga yaliyofanyika katika uwanja mdogo wa Olimpique du Sousse, kwa bahati mbaya wakati wanafika uwanjani hapo wachezaji wa Yanga walikuwa wakisoma dua ya kumaliza mazoezi.
No comments:
Post a Comment