Wednesday, June 24, 2015

usemavyo ubongo wa Kakore: Nooij alijifukuza kabla ya kufukuzwa




KOCHA wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ aliyefukuzwa, Mart Nooij, ni miongoni mwa watu waliopewa kipaumbele kwenye vyombo vya habari nchini Tanzania kwa muda wa wiki mbili ingawa kwa wiki iliyopita na mwanzoni mwa wiki hii nguvu hiyo iliongezeka.
Sababu za kupewa nafasi kubwa kwenye vyombo vya habari na midomoni mwa wapenzi na mashabiki wa soka la Tanzania, ni kutokana na Taifa Stars kufanya vibaya katika mechi tano mfululizo jambo ambalo halikuwa la kawaida kwa muda wote wa zaidi ya miaka 50 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kiukweli kocha huyu inawezekana alikuwa bora lakini kwa mwelekeo wa soka letu na mfumo wa soka letu alikuwa haendani nao, kwa kifupi ni kwamba, viatu alivyokuwa amevivaa vilikuwa havukumtosha.
Lakini jambo kubwa ambalo nililiona kwa Nooij, ni kukosa hamasa na ukaribu na wenye timu yao yaani Watanzania wenyewe, ndiyo sababu timu ilikosa hamasa  kama ilivyokuwa wakati wa Marcio Maximo na waliokuja baada yake; Jan Poulsen na Kim Poulsen.
Kosa hili lilikuwa wazi kwani Nooij alisahau kuwa Stars ni timu ya umma jambo lililomfanya kuiweka timu mbali na wenye timu, hili ndilo lilikuwa kosa la kwanza kwani hata alipokosea kidogo kwenye uwanja mashabiki hao walikuwa wa kwanza kumlaumu na kumkosoa.
Makosa ya aina hii hakuna kocha anayeweza kudumu kwenye timu za taifa kwani ninachofahamu mimi ni kwamba, moja ya sifa ya kocha wa timu ya taifa ni kuhakikisha inakuwa ni mali ya watu na si mali ya mtu.
Jambo lingine ni kushindwa kuwatumia makocha wazawa kwa ufasaha, hili limekuwa ni tatizo kubwa kwa makocha wengi wa kigeni wanaokuja kufanya kazi ingawa wale wanaowatumia wazawa wamekuwa wakifanikiwa.
Kwa mfano, Maximo aliweza kuwatumia makocha kama Juma Pondamali, Ally Bushiri, marehemu Sylverster Mash, ambao walikuwa wakilifahamu vyema soka la Tanzania kwani wamekuwa ni sehemu ya soka hilo.
Lakini angalia makocha waliokuja kwenye ngazi za klabu akiwemo Patrick Phiri alikuwa na wasaidizi wazawa akiwa na kikosi cha Simba na hata kocha wa sasa wa Yanga, Hans van der Pluijm pamoja na mafanikio yake ndani ya timu hiyo, amekuwa akitegemea uwepo wa makocha, Charles Mkwassa na kocha wa makipa, Juma Pondamali.
Mfumo huu ndio umewafanya makocha wengi duniani kufanikiwa, lakini ilikuwa kinyume kwa Nooij ambaye alikuwa akiamini katika kile anachokifahamu na naamini alikuwa hashauriwi vyema na wale waliokuwa wakimsaidia.
Hivyo kwa Nooij naye alitakiwa kuangalia mbali au kama wanavyosema vijana wa siku hizi alitakiwa kujiongeza zaidi na kuangalia mbali kwa kushirikisha katika kazi zake makocha wazalendo, lakini nasikitika kuwa pamoja na wingi wa makocha bora hawajatumika inavyostahili.
Hili limekuwa ni kosa ambalo limemgharimu Nooij na iwapo akija kocha mwingine kutoka nje ya Tanzania akipewa jukumu hilo kwa siku za baadaye lazima aambiwe ukweli wa jambo hili kwa maana akidharau atashindwa tena.
Lakini mwisho wa yote ni kwamba, lazima tukubaliane kuwa nchi yetu inahitaji kubadilisha mfumo wa soka na uendeshaji wake kwani bado tupo kwenye mfumo wa kizamani ambao hauwezi kutuvusha.
Miongoni mwake ni pamoja na kuimarisha soka la vijana na watoto kwani ndiko kwenye mtaji na maendeleo kwa soka letu na si jambo lingine lolote.
Hapa ndipo tulipokosea, lakini nikiangalia makocha wapo na wanaweza kutuvusha ila lazima tukubaliane kuwa hawa hawajatumika ipasavyo na kama likifanikiwa hili tunaweza kusogea mbele lakini si kwa aina ya kocha kama Nooij kutokana na msimamo wake na aina ya utendaji wake wa kazi.   
Kwa sababu hiyo, ninachokiona ni kwamba, Nooij alijifukuza kabla ya kufukuzwa kwenye kikosi cha timu ya taifa kwa kushindwa kuangalia alama za nyakati na wale waliomzunguka na kufanya naye kazi.

No comments:

Post a Comment