Wednesday, June 24, 2015

Muuaji wa Stars awaita Simba Taifa


NA MWANDISHI WETU
STRAIKA Mganda, Erisa Ssekisambu ambaye ndiye aliyeifunga mabao 2 kati ya 3 yaliyoitoa Taifa Stars katika mbio za  kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan), amewataka matajiri wa Simba, kufika kwenye Uwanja wa taifa kushuhudia muziki wake.
Mganda huyo anayekipiga katika klabu ya SC Villa atakuwepo jijini Dar es Salaam akiambatana na timu yake inayokuja kucheza mechi ya tamasha maalum la kuzuia Mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) Jumamosi katika Uwanja wa Taifa.
Ssekisambu amewaalika Simba baada ya kupata taarifa kwamba viongozi wa timu hiyo wameanza mbio za kusaka saini yake, ikiwa ni siku chache baada ya Shirikisho la soka nchini TFF kuridhia kuongeza idadi ya wachezaji wa kigeni kutoka watano hadi saba.
Akizungumza na toka nchini Uganda, Ssekisambu alisema endapo Simba watafika uwanjani na kuridhishwa na kiwango chake na pia watafikia makubaliano na viongozi wake basi hatokuwa na kikwazo cha kuvaa jezi nyekundu msimu huu na kuungana na Mganda mwenzake Emmanuel Okwi anayekipiga Simba.
Simba imo katika mawindo ya wachezaji watakaokiimarisha kikosi chake, ambapo juzi Rais wa klabu hiyo Evans Aveva alisema wanataka kufanya mapinduzi makubwa ya soka msimu huu kwa kusajili wachezaji wazuri na wenye uwezo watakaoirudishia ubingwa timu hiyo ya Msimbazi.
Msimu uliopita Simba haikufanya vizuri katika michuano ya Ligi Kuu ambapo licha ya kusajili nyota watano wa nje lakini ilishindwa kufurukuta na kujikuta ikimaliza ligi hiyo ikishika nafasi ya tatu.

No comments:

Post a Comment