Wednesday, August 19, 2015

Yanga acha kabisa



 NA MSHAMU NGOJWIKE
 YANGA acha kabisa! Jeshi kamili la timu hiyo limewasili jana jijini Dar es Salaam likiwa limejidhatiti kisawasawa baada ya kuweka kambi ya wiki mbili jijini Mbeya likijiwinda na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC.
 Mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara, watacheza na Azam FC katika mchezo huo wa Ngao ya Jamii utakaopigwa Jumamosi wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo unasubiriwa kwa hamu kutokana na ukweli kwamba kwa siku za hivi karibuni timu hizo zimekuwa na uhasimu wa jadi kama inavyokuwa kwa mechi ya Simba na Yanga. 
Yanga iliweka kambi ya wiki mbili Tukuyu mjini Mbeya ikijifua kikamilifu kuhakikisha inamalizia hasira zake zote kwa Wanalambalamba hao ambao waliwafunga katika mchezo wa robo fainali michuano ya Kagame.
Wakiwa Mbeya, Wanajangwani hao waliweza kutembeza kichapo cha hatari kwa timu za mkoa huo zilizojipendekeza kutaka kucheza nayo bila kujua wana hasira na Azam.
 Katika mechi hizo, Wanajangwani hao walianza kutembeza kichapo kwa Kimondo FC ya Mbozi inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza cha mabao 4-1 mchezo ukichezwa Uwanja wa CCM Vwawa.
 Baada ya hapo mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, waliwachapa maafande wa Prisons ya Mbeya kwa mabao 2-0, kabla ya kuhitimisha kambi yao kwa ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Mbeya City.
 Katika kambi hiyo ya Mbeya, Kocha wa Yanga, Hans Van Der Pluijm, alionekana kuwa mbogo baada ya kutoa dozi ya mazoezi ya kufa mtu kiasi cha kuonyesha kuwa wamepania kuibuka na ushindi katika mchezo huo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam.
 Kitu ambacho kimeibua hisia za watu wengi ni kitendo cha wachezaji wa Yanga kuendelea na mazoezi ya kupasha misuli baada ya kocha kumaliza programu jambo linaloashiria hatari kwa timu yoyote pinzani watakayokutana nayo.
 Wakati Yanga ikijinasibu kufanya vizuri katika mchezo huo wa Ngao ya Jamii, kwa upande wao Azam wameibuka na kuchimba mkwara mzito wakidai kuwa wembe waliowanyolea Kagame wameuongezea makali.
 Azam ilijichimbia visiwani Zanzibar ambako iliendeleza wimbi la ushindi chini ya kocha wake Mwingereza, Stewart Hall, ambapo kikosi hicho kimeshinda michezo 12 tangu kocha huyo kukabidhiwa majukumu hayo.
 Wakiwa Zanzibar waliweza kushinda michezo yao yote mitatu ya kirafiki wakianza kutoa kipigo cha bao 1-0 dhidi ya KMKM.
 Mchezo uliofuata waliongeza dozi kwa kuwafunga Mafunzo mabao 3-0 kabla ya kuhitimisha kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya maafande wa JKU.
 Kwa ujumla katika mechi zote 12 chini ya Stewart tangu arejee Juni mwaka huu, Azam imefungwa mabao mawili tu katika mechi ya kwanza kabisa dhidi ya Friends Rangers Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
 Baada ya hapo, nyavu za Azam hazijaguswa tena kuanzia kwenye mechi za kirafiki hadi Kombe la Kagame pamoja na hizi tatu za kirafiki Zanzibar ambazo makipa wa Azam hawajaokota mpira nyavuni. 
 Kutokana na maandalizi ya timu zote mbili ni wazi mchezo huo utakuwa wa aina yake ukitarajiwa kuhudhuriwa na mashabiki wengi ili kujua nani mbabe kwa mwenzake.
 Kihistoria hiyo itakuwa mechi ya nane ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya tatu kuzikutanisha timu hizo.
 Kwa mara ya kwanza timu hizo zilikutana mwaka juzi na Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0, mfungaji akiwa ni Salum Telela, mwaka jana tena Yanga ikaibuka na ushindi wa mabao 3-0, ambapo mawili yalifungwa na straika Mbrazil, Geilson Santona 'Jaja' na moja la Simon Msuva.

No comments:

Post a Comment