Wednesday, August 19, 2015

Kerr airudisha Simba ya 2003



Kikosi cha Simba cha mwaka 2003, kutoka kushoto waliosimama ni  Emmanuel Gabriel,****,  Muso, Alex, Victor Costa, Suilman Matola, waliochuchumaa kutoka kushoto, Ramadhan Waso, Ulimmboka Mwakingwe, Juma Kaseja, Athuma Machupa na Boinicafe Paswasa.

NA EZEKIEL TENDWA
 UNAIKUMBUKA ile Simba ya mwaka 2003? Ilikuwa timu hatari ambayo ilitingisha bara hili la Afrika hasa baada ya kuwavua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa, Zamaleck ya Misri na kuleta shangwe kwa mashabiki na Watanzania kwa ujumla.
 Kwa sasa mashabiki wa Simba wanayo kila sababu ya kuanza kutabasamu baada ya kikosi hicho kuwa moto wa kuotea mbali ikipikwa vya kutosha na kocha wake mkuu, Dylan Kerr na haitakuwa ajabu zama zile zikarejea tena.
 Simba ile ya 2003 ambayo ilikuwa chini ya kocha kutoka Kenya, James Siang’a, ilisheheni wachezaji hatari kila idara kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili, Evans Aveva ambaye kwa sasa ni Rais wa klabu hiyo.
Uongozi wa Simba kwa sasa chini ya Aveva wameanza kuweka mipango kabambe ya kuhakikisha kikosi chao kinaanza kuonyesha makucha yao wakipania kuibuka mabingwa msimu unaokuja ili kufanikiwa kucheza michuano ya kimataifa. 
Kwa misimu mitatu mfululizo Simba wameshindwa kumaliza moja ya nafasi za juu na sasa wameweka wazi kwamba wataingia katika ligi wakiwa nguvu moja ili kupata kile ambacho wamekikosa kwa muda mrefu.
Katika michezo yake ya kirafiki wameonyesha kandanda la kuvutia wakiibuka na ushindi wa bao 1-0 katika tamasha la Simba Day dhidi ya SC Villa ya Uganda na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya URA pia ya Uganda michezo yote ikichezwa Uwanja wa Taifa.
 Kamati ya usajili ya Simba chini ya Zacharia Hanspope na msaidizi wake, Kasim Dewji, wamekuwa wakihangaika huku na kule kuhakikisha wanapata wachezaji wazuri watakaokidhi matakwa na benchi la ufundi kitu ambacho kwa kiasi fulani wamefanikiwa.
Simba ya mwaka 2003 ilikuwa chini ya mwenyekiti wake, Ahmed Balozi, Katibu mkuu akiwa Kasim Dewji ambaye kwa sasa ni msaidizi wa Hanspope katika kamati ya usajili, huku Aveva ambaye kwa sasa ni Rais wa klabu hiyo alikuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili.
Kikosi hicho ambacho kiliwatoa mabingwa watetezi wa ligi hiyo ya mabingwa Afrika, Zamalek, kiliundwa na mlinda mlango, Juma Kaseja, Said Sued, Ramadhan Wasso, Boniface Pawasa, Victor Costa, pamoja na Seleman Matola aliyekuwa nahodha ambaye kwa sasa ni kocha msaidizi.
Wengine walikuwa Athuman Machupa, Christopher Alex ambaye kwa sasa ni marehemu, Emmanuel Gabriel, Yusuph Macho ‘Musso’, pamoja na Ulimboka Mwakingwe ambapo katika mechi ya kwanza iliyopigwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Katika mchezo wa marudiano Simba ilifungwa bao 1-0 na kuzifanya timu hizo ziende kwenye penalti ambapo mlinda mlango, Juma Kaseja aliokoa moja huku Christpher Alex 'Massawe' akifunga penalti ya mwisho na kupeleka shangwe mitaa ya Msimbazi.


No comments:

Post a Comment