Wednesday, September 9, 2015

Yanga yaanza tizi maalumu

NA SALMA MPELI
KAZI imeanza! Zikiwa zimesalia siku tatu kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kikosi cha mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga, kimeanza kufanya tizi maalumu kwa ajili ya mechi yake ya kwanza dhidi ya Coastal Union ya Tanga, itakayoanza kukipiga nayo Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Mechi hiyo inapigwa huku Yanga ikiwa na kumbukumbu ya kuwafunga Coastal Union mabao 8-0 katika mechi ya mwisho kuzikutanisha timu hizo msimu uliopita.
Yanga, ambayo iliachana na mpango wa kuweka kambi Bagamoyo kwa ajili ya mechi hiyo, imeamua kujifua kwenye uwanja wake wa Kaunda kwa kocha wake, Hans van Pluijm kuwapa wachezaji tizi maalumu baada ya wachezaji wote wa kikosi kizima kutimia.
Hatua hiyo imekuja baada ya kikosi cha timu hiyo kukamilika kutokana na wachezaji wake tisa waliokuwa kwenye vikosi vyao vya timu za Taifa kurejea na kujiunga na timu hiyo katika mazoezi yaliyoanza jana kwenye Uwanja wa Kaunda.
Wachezaji hao ni pamoja na Ally Mustafa 'Barthez,' Kelvin Yondan, Nadir Haroub 'Cannavaro,' Simon Msuva, Deus Kaseke, Haji Mwinyi ambao walikuwa katika kikosi cha Taifa Stars, huku wachezaji Haruna Niyonzima akiwa na timu yake ya Taifa ya Rwanda, Vicent Bosou akiitumikia Togo, pamoja na Amis Tambwe aliyekuwa na timu yake ya Taifa ya Burundi.
Akizungumza na DIMBA Jumatano, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema tayari wachezaji hao wote waliokuwa kwenye timu zao wamesharejea nchini na kuanza mazoezi ya pamoja jana, isipokuwa Niyonzima ambaye alitarajiwa kuwasili jana jioni.
Awali Yanga walikuwa wakifanya mazoezi asubuhi tu, lakini baada ya kikosi kizima kukamilika kwa sasa dozi imeongezeka na wanafanya kutwa mara mbili, yaani asubuhi na jioni.
Akizungumzia kuhusu kukacha mpango wa kwenda Bagamoyo, Hafidh alisema wameamua kubaki jijini Dar es Salaam wakiamini kuwa wanaweza wakapata kile wanachokihitaji wakiwa hapahapa.
Hiyo ni kambi ya pili kuahirishwa na klabu hiyo kwenye maandalizi yao msimu huu, ambapo awali walipanga kujichimbia visiwani Zanzibar, lakini baadaye mipango hiyo ikayeyuka.

"Tumeona hakuna haja ya kwenda tena Bagamoyo, timu itabaki hapa na kuendelea na ratiba yake ya mazoezi katika Uwanja wa Kaunda na tayari kikosi kimekamilika baada ya wachezaji wote kurejea na itakuwa ikifanya mazoezi asubuhi na jioni,"  alisema Hafidh.
Alisema, kikosi chao kipo vizuri na wana imani wataanza kwa kutoa dozi kwenye mchezo huo wa kwanza na kuendeleza ushindi kwenye mechi nyingine.
Wanajangwani hao wamepania kupata pointi tisa katika michezo yao mitatu ya kwanza dhidi ya Coastal Union, Tanzania Prisons na JKT Ruvu, kabla ya kuvaana na watani wao wa jadi, Simba katika mechi ya nne.
Yanga imefanikiwa kufungua vizuri msimu mpya wa Ligi Kuu Bara, baada ya kufanikiwa kutwaa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam, mchezo uliopigwa Septemba 22, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment