Wednesday, September 9, 2015

Pointi 11 za Stars kuelekea Afcon hizi hapa

TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Jumamosi iliyopita ilishindwa kupata pointi tatu nyumbani mbele ya Nigeria, mchezo ambao ulikuwa ni wa kufuzu kwa michuano ya Afrika (Afcon) mwaka 2017.

Binafsi niwapongeze wote waliofanikisha kupatikana kwa matokeo ya sare kutokana na ukweli kwamba Nigeria ni timu kubwa na yenye jina Afrika na duniani kote.

Pongezi hizi ziende kwa wachezaji waliojitoa kwa hali na mali kuhakikisha kuwa wanapata ushindi ingawa matokeo hayakuwa hivyo kama walivyotaka au kama ilivyokuwa kiu ya Watanzania walio wengi akiwemo mimi mwenyewe niliyetarajia Nigeria ingenyolewa kwenye Uwanja wa Taifa.

Hii ina maana kwamba, dawati la ufundi linaloongozwa na Kocha Charles Mkwasa na msaidizi wake Hemed Morocco, wamefanya kazi kubwa kuhakikisha kuwa kikosi kinapata matokeo bora na japo haikuwa hivyo lakini pointi moja si haba kwani tayari ndiyo mwelekeo bora wa kufika katika mafanikio.

Nikiangalia kikosi cha Stars bado kina nafasi kubwa ya kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Afcon iwapo kikifanikiwa kupata pointi 10 muhimu ambazo mimi naamini ndizo zinazoweza kusaidia kuwa na uhakika wa kupata nafasi mbili za juu.

Baada ya kupoteza kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Misri, lakini naamini itafanikiwa kushinda mechi mbili dhidi ya Chad ambapo mchezo wa kwanza itakuwa ni Machi 26 mwakani na itakuwa ni mechi ya ugenini.

Kwa maana hiyo, Stars itahitaji kupata pointi hizo tatu ili kuwa na pointi nne mkononi kabla ya kucheza mechi za marudiano wiki inayofuata yaani itakuwa Machi 28 mwaka 2016 hivyo michezo hiyo miwili lazima Stars ipate ushindi.

Ikifanikiwa kunyakua pointi sita kutoka Chad utakuwa ni mtaji mkubwa kuelekea michuano ya Afcon kwani tayari wababe wawili, Misri na Nigeria watakuwa wameshakutana na kurejeana hivyo mwanga wa nani atakayekwenda na atakayebakia utakuwa umeshaanza kuonekana.

Kwa mazingira hayo naamini kuwa mikakati ikianzia sasa hili ni jambo linalowezekana na Stars ikavunja mwiko wa kutoshiriki michuano hiyo kwa zaidi ya miaka 30 sasa.

Mechi nyingine muhimu ambayo naamini inaweza kuwa sehemu ya mtaji kwetu kama Watanzania ni ile ya Juni 4 mwaka 2016, ambapo Stars itakuwa ikicheza na Misri kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Mchezo huu ni muhimu zaidi kwa sababu Stars inahitajika kushinda kwa gharama yoyote iwavyo hali itakayoifanya kuwa na pointi 10 kwani itakuwa imeshinda mechi tatu sawa na pointi tisa ambazo ukijumlisha na pointi moja iliyonayo kwa sasa tayari mwelekeo utakuwa ni mzuri.

Vile vile mchezo wa Tanzania na Nigeria utakaopigwa Septemba 2 mwaka 2016 jijini Lagos, utakuwa ni wa kukamilisha ratiba tu lakini Stars ikihitaji kupata japo pointi moja tu ili kuwa na pointi 11 ambapo itakuwa ni mtaji mkubwa kwao.

Stars ambayo ipo Kundi G kwa sasa inashika nafasi ya tatu baada ya kucheza mechi mbili ikitoa sare moja, ikifungwa moja ambapo haijafunga bao lolote lakini ikifungwa mabao matatu ikiwa na pointi moja.

Misri ndiyo inayoongoza kundi hilo ikiwa na pointi sita baada ya kucheza mechi mbili na kushinda zote huku ikiwa imefunga mabao nane ikifungwa bao moja na huku Nigeria ikishikilia nafasi ya pili kwa kucheza mechi mbili ikishinda moja na kupata sare moja huku ikiwa na pointi nne.

Kwa mwelekeo huu hadi sasa bado naona uwezo wa kupata nafasi mbili za juu kwa Stars ni mkubwa kwani kwa hesabu nilizoainisha hapo awali ni wazi kuwa nafasi yao si mbaya ila kinachotakiwa ni mipango endelevu.

Ninachokiona cha haraka kinachoweza kufanyika kwa wakati huu ni mikakati iliyopo iendelezwe ikiwemo kupatikana kwa mechi za kirafiki za mara kwa mara kabla ya mwezi Machi mwakani kwa maana angalau kila mwezi ipatikane mechi moja ngumu ya kirafiki.

Baadhi ya mechi ambazo naamini zinaweza kuwa msaada mkubwa ni kucheza ugenini na nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Tunisia, Angola, Mali au Togo na ikiwa mechi za ugenini inaweza kuwa msaada mkubwa zaidi kwa Stars ili wachezaji wake waweze kupata uzoefu kwenye mechi za ugenini.

Hizi ndizo hesabu zangu ambazo naamini zitaweza kuwa msaada kwa nchi yetu kwani pointi 10 zinawezekana kupatikana kama dhamira ikiwepo kama ambavyo ilionekana Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa.

No comments:

Post a Comment