Tuesday, October 27, 2015

Busungu, Maguli waitwa Stars

Busungu 
 
KOCHA wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Charles Boniface Mkwasa, jana alitangaza kikosi cha timu hiyo kitakachovaana na Algeria, huku akiwaita mastraika wanaotisha kwa kutupia nyavuni, Malimi Busungu wa Yanga na Elius Maguli wa Stand United waje kukinogesha.
Stars na Algeria zinatarajia kuvaana Novemba 14 jijini Dar es Salaam katika mechi ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia zinazotarajiwa kufanyika jijini Moscow, Russia, mwaka 2008.
Timu hiyo imefanikiwa kuvaana na Algeria katika hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania kupangwa kwenye makundi baada ya kuitoa Malawi katika hatua ya kwanza.
Mkwasa amemuongeza Maguli ambaye amekuwa katika kiwango bora kwenye msimamo wa wafungaji bora wa Ligi Kuu Bara, akiwa na mabao nane wakati Busungu yeye akiwa na mchango mkubwa katika kikosi cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga, ambapo pia amefunga mabao mawili kwenye msimamo wa wafungaji wa ligi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam, Mkwasa ametaja wachezaji 28 ambao watakwenda kambini Oman Novemba 2, mwaka huu.
Mkwasa amewataja wachezaji wengine walioitwa kuwa ni makipa, Aishi Manula (Azam FC), Ally Mustafa 'Barthez' (Yanga SC) na Said Mohammed (Mtibwa Sugar).
Mabeki ni Shomary Kapombe (Azam FC), Juma Abdul, Mwinyi Hajji Mngwali, Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondan (Yanga SC), Hassan Ramadhan Kessy, Mohammed Hussein 'Tshabalala,' Hassan Isihaka (Simba SC) na Salim Mbonde (Mtibwa Sugar).
Viungo ni Himid Mao, Mudathir Yahya, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Frank Domayo (Azam FC), Jonas Mkude, Said Ndemla (Simba SC) na Salum Telela (Yanga SC), wakati washambuliaji ni Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC), Mrisho Ngassa (Free State Stars, Afrika Kusini), Farid Mussa, John Bocco (Azam FC), Simon Msuva, Malimi Busungu (Yanga SC), Elias Maguli (Stand United) na Ibrahim Hajib (Simba SC).
"Kikosi hicho kitaingia kambini Novemba 1 katika hoteli ya Urban Rose, Dar es Salaam, kabla ya safari ya Muscat, Oman kwa kambi ya siku 10.
"Tukiwa Oman, pamoja na mazoezi, tutacheza mchezo mmoja au miwili ya kujipima na wenyeji wetu, iwapo watakuwa tayari kabla ya kurejea Dar es Salaam Novemba 11 tayari kwa mchezo wa kwanza na Algeria Novemba 14, Uwanja wa Taifa,” alisema Mkwasa.
Alisema kikosi hicho kitaondoka Dar es Salaam kwenda Algiers Novemba 16 mwaka huu, tayari kwa mchezo wa marudiano Novemba 17, nchini Algeria.

No comments:

Post a Comment