KOCHA Mkuu wa Yanga Mholanzi, Hans Pluijm, ana
hasira za msimu uliopita kushindwa kuifikisha timu hiyo pazuri kwenye michuano
ya kimataifa lakini safari hii ameapa lazima kieleweke.
Unajua kwanini? Mholanzi huyo safari hii amepeleka
Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), majina ya silaha zake 24 huku 10 zikiwa
za kimataifa tayari kwa kufanya makubwa mapema Februari mwakani kwenye michuano
ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika majina hayo 24 ukiwaacha, Thaban Kamusoko,
Donald Ngoma, Amissi Tambwe, Haruna Niyonzima, Issoufou Boubacar Garba, Vicent
Bossou na Mbuyu Twite, Pluijm ameamua kuleta majembe mengine mawili ya
kimataifa ingawa tayari inaye mchezaji mmoja Mnyarwanda, Jerome Sina,
anayefanyiwa majaribio.
DIMBA Jumatano limethibitishiwa kwamba Yanga
itawaleta straika, Spencer Sautu kutoka Ashanti Gold ya Ghana, ambaye ataungana
na beki shupavu aitwae Kabongo kutoka Congo (DRC).
Wawili hao wanakuja wakati wowote nchini kuanzia
sasa kufanya majaribio ingawa inaelezwa kwamba kocha Hans anavifahamu vyema
viwango vyao vya soka.
Chanzo cha habari cha uhakika kimelieleza gazeti
hili kuwa ujio wa wawili hao utafanya timu hiyo iwe na wachezaji 10 wa
kimataifa ili kukifanya kikosi chao kiweze kuhimili vishindo vya michuano hiyo
mikubwa zaidi barani Afrika na yenye utajiri mkubwa inayoandaliwa na CAF.
Aidha, chanzo hicho kilieleza kuwa Yanga bado
inaendelea kumfanyia majaribio kiungo wa Rayon Sport, Jerome Sina, ingawa
usajili wake utasubiri kwanza ili kulinganishwa kiwango na Sautu.
Jerome mwenye miaka 26 raia wa Congo (DRC) amemvutia
Pluijm na inaelezwa iwapo atafuzu majaribio atasajiliwa mwishoni mwa msimu kwa
ajili ya kuibeba Yanga.
"Sasa hivi hatutaki masihara kwani tunahitaji
kufika mbali zaidi, ukiangalia msimu uliopita hatukufikia malengo yetu kwa vile
tulitolewa mapema ndiyo maana usajili wa wachezaji wa kigeni unafanyika kwa
umakini mkubwa tukiamini watasaidiana vyema na wazawa ili mwakani tuweze
kuvunja rekodi yetu," alisema mtoa habari.
Alisema tayari benchi la ufundi la timu hiyo limependekeza
kupeleka idadi ya majina 24 kwa ajili ya michuano hiyo ya kimataifa ambapo
wachezaji hao wawili wanaotarajia kutua hapa nchini wataungana na Sina kwa
ajili ya majaribio na baadaye kusaini.
Katika hatua nyingine, Yanga imebadilisha mipango
yake ya kwenda kujifua nchini Ghana kwa ajili ya kujiandaa na michuano hiyo na
badala yake watabaki hapa nchini na kuzialika timu za nje ili kucheza nazo
mechi za kujipima.
Kocha wa Yanga, Hans Van Der Pluijm, ameliambia
DIMBA Jumatano kuwa wana mpango wa kuzialika timu tatu za kimataifa ambazo ni
Ashanti Gold ya Ghana pamoja na Gor Mahia na KCB zote za Kenya.
"Mpango wetu wa kwenda nje ya nchi umekufa
kutokana na ratiba kuingiliana, lakini tumezialika timu nne ambapo mbili za KCB
na Gor Mahia tayari zimethibitisha huku Ashanti ikiwa bado," alisema kocha
huyo.
No comments:
Post a Comment