NA ZAINAB IDDY
LICHA ya mshambuliaji wa Simba, Hamis Kiiza, kuongoza katika mbio za ufungaji bora, mfungaji bora wa msimu uliopita, Simon Msuva wa Yanga, amesema kwamba Mrundi, Amis Tambwe, ndiye atakayeibuka mfungaji bora msimu huu.
Msuva amelisema kwamba, licha ya Tambwe kupata upinzani mkali kutoka kwa Kiiza, lakini ana nafasi kubwa ya kupata tuzo hiyo msimu huu kutokana na uwezo wake wa kupachika mabao.
“Najua upinzani katika mbio hizo za ufungaji bora ni mkubwa lakini kwangu mimi nampa nafasi kubwa Tambwe kwani anao uwezo mkubwa wa kutumia nafasi anazozipata,” alisema Msuva.
Tambwe ambaye msimu wa 2013/14 aliibuka mfungaji bora akiwa na mabao 17 wakati huo akiichezea Simba, kwa sasa ana mabao 17, nyuma ya Kiiza mwenye mabao 19.
Katika msimu uliopita, Msuva alifanikiwa kutwaa tuzo ya ufungaji bora baada ya kuifungia timu yake jumla ya mabao 17 akifuatiwa na Tambwe aliyetikisa nyavu mara 15.
No comments:
Post a Comment