Tuesday, April 12, 2016

Yanga SC yapata dawa ya Waarabu



NA EZEKIEL TENDWA
KAMA ulidhani safari ya Yanga katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ndio imefikia tamati baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani, imekula kwako kwani Wanajangwani hao wamekuja na mbinu kali kuwamaliza Waarabu hao nyumbani kwao.
Unajua ikoje? Kocha Mkuu wa kikosi hicho Mholanzi, Hans Van De Pluijm, amechunguza kwa umakini kikosi chake na udhaifu uliojitokeza katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Taifa na sasa ndio anaufanyia kazi.
Katika mchezo wa kwanza uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Yanga walilazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na sasa Pluijm anataka kuishangaza Afrika kwa kuwaadhibu Waarabu hao tena wakiwa uwanja wao wa nyumbani.
Licha ya kwamba wadau wengi wa soka wanaamini Yanga wana mlima mrefu wa kupanda baada ya matokeo hayo ya sare Uwanja wa Taifa, kocha Pluijm alishaweka wazi kuwa kazi bado ni mbichi.
Pluijm ana uhakika wa kikosi chake kuibuka na ushindi katika mchezo huo hasa baada ya baadhi ya wachezaji wake waliokuwa majeruhi kama Mbuyu Twite kupona huku akiwa na uhakika wa kumtumia kiungo mwenye vitu vingi uwanjani, Haruna Niyonzima ambaye alikosa mchezo wa kwanza kutokana na kutumikia adhabu ya kadi mbili za njano.
Katika mchezo huo wa marudiano, Yanga watahitaji ushindi wowote ule au hata kutoka sare ya kufungana kuanzia mabao 2-2 lakini kama wakitoka sare ya bao 1-1 ni dhahiri timu hizo zitakwenda hatua ya kupigiana mikwaju ya penalti.
Kwa kulitambua hilo, Pluijm ameanza kuwaandaa wachezaji wake katika zoezi la upigaji penalti ambapo kwenye mazoezi ya jana yaliyofanyika viwanja vya Gymkana, kocha huyo alikuwa akiwapa mbinu za penalti.
Pluijm anakumbuka msimu wa 2014 ambao walitolewa na Al Ahly hao hao kwa mikwaju ya penalti na sasa hataki jambo hilo lijirudie tena kwani dhamira yake ni kuhakikisha msimu huu anawatia adabu Waarabu hao.
Waliopiga penalti hizo msimu huo wa 2014 na kukosa ni Oscar Joshua, Mbuyu Twitte, pamoja na Said Bahanuzi ambaye kama penalti yake ingeingia Yanga wangetinga moja kwa moja hatua inayofuata.
Waliopata penalti hizo walikuwa ni Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Didier Kavumbagu, pamoja na Emmanuel Okwi ambao hawapo kwa sasa katika kikosi hicho isipokuwa Cannavaro ambaye anaendelea kudunda.
Mbinu nyingine ambayo Wanajangwani hao watakwenda kuitumia ni kuhakikisha wanashambulia mwanzo mwisho kwani wanajua kuwa kitakachowaweka salama ni kuibuka na ushindi au kutoka sare ya zaidi ya mabao 2-2 vinginevyo watatupwa nje ya michuano hiyo.
Al Ahly, klabu inayoongoza kwa ubora barani Afrika ikiwa imetwaa ubingwa huo mara nane, inasaka ubingwa na kutaka kuendelea kuwa wafalme wa Afrika, hatua ambayo ndiyo itaingiza fedha zaidi kupitia kwenye matangazo na udhamini.
Yanga yenyewe inatafuta kufuzu kwa mara ya pili kwenye hatua ya makundi baada ya kufanya hivyo mwaka 1998, ambapo ilishika nafasi ya nne kwenye Kundi B na zawadi yake ya Dola 40,000 ikaishia mifukoni mwa wajanja wa kilichokuwa Chama cha Soka Tanzania (FAT). Licha ya Kamati ya Muda ya Tarimba Ghullam Abbas kupiga kelele, mpaka leo haijulikani ni nani hasa aliyefaidika nazo.
Licha ya kuwania Dola 400,000 hata kama itashika mkia kwenye kundi lake, lakini kushiriki hatua ya makundi kutaipa Yanga fursa ya kupata matangazo pamoja na kuongeza ubora wake barani Afrika.
Hata hivyo, Yanga ikifuzu hatua hiyo inaweza kuogelea kwenye utajiri mkubwa endapo itafanya vizuri pia, kwani zawadi zinatamanisha ambapo mshindi wa tatu kwenye kila kundi ataondoka na kitita cha Dola 500,000 (takribani Sh bilioni 1.05) wakati ambapo timu zitakazofuzu kucheza nusu fainali kila moja italamba Dola 700,000 (takribani Sh bilioni 1.47) ambao ni utajiri mkubwa unaoweza kusaidia kuweka mipango madhubuti ya kuendeleza klabu kwa kuimarisha programu ya soka la vijana.
Kwa mujibu wa CAF, bingwa wa mashindano hayo atajinyakulia kitita cha Dola milioni 1.5 (karibu Sh bilioni 3.15) huku mshindi wa pili akipata Dola milioni moja (Sh bilioni 2.1).
Hizi ni fedha nyingi, lakini haziwezi kuja kirahisi rahisi kwa sababu zinahitaji uwekezaji wa kutosha katika maandalizi ya timu pamoja na kuwa na mipango endelevu.
Kwa mujibu wa kanuni za CAF, hata kama Yanga itatolewa katika hatua hii, basi itaingia kwenye hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho kucheza na timu nane ambazo zitafuzu na ikishinda itaingia kuwania utajiri mwingine.
Katika kuhakikisha Waarabu hao wanatolewa katika michuano hiyo mchana kweupe, uongozi wa Yanga nao umeliunga mkono benchi la ufundi ambapo wameandaa kitita kikubwa cha fedha kwa ajili ya mchezo huo.
Taarifa za uhakika ambazo DIMBA imezinasa zinadai kuwa uongozi huo umeandaa milioni 220 ambazo ni kwa ajili ya usafiri kwa wachezaji na mashabiki wao pamoja na hoteli watakayofikia ikiwamo pia posho.
Taarifa hizo zinadai kuwa Wanajangwani hao hawataki kuhudumiwa kwa kitu chochote na wenyeji wao hao watakapofika huko Misri ili kuepuka aina yoyote ya hujuma ndiyo maana wameamua kujihudumia wenyewe kila kitu.

No comments:

Post a Comment