KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Mart Nooj amesema kuwa kikosi chake kipo
vizuri na kitaweza kushinda mchezo wa kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON)
mwakani nchini Morocco dhidi ya Msumbiji ‘Mambas’.
Nooj alisema kuwa timu inatarajiwa kuondoka leo jijini kwenda
kuweka kambi nyingine Tukuyu, mkoani Mbeya ambapo itarejea siku tatu kabla ya
mechi.
Akizungumzia kambi ya Botswana alisema, ilikuwa nzuri na
imesaidia kuwajenga kutokana na kufanya mazoezi na kupata mechi tatu za
kujipima nguvu.
Amesema katika mechi hizo, walifungwa mbili, moja dhidi ya
timu ya taifa ya Botswana mabao 4-2 na nyingine dhidi ya timu ya Jeshi la
nchini humo, BDF walishinda moja 3-1 na kufungwa moja 2-1.
Katika hatua nyingine wachezaji wawili wa timu hiyo Jonas
Mkude na Himid Mao ni majeruhi ambapo Daktari wa timu hiyo Bile Haonga alisema kwamba wamefanyiwa vipimo na wanaendelea na
uangalizi.
Kwa upande wake nahodha wa timu hiyo Nadir Haroub ‘Cannavaro’
alisema kuwa wamejifunza mengi katika kambi ya Botswana, na kufungwa kwao mechi
mbili kati ya tatu walizocheza ni uzembe kwenye safu ya ulinzi.
“Kikubwa ni Watanzania kuendelea kutuunga mkono maana mpira
unabadilika na tunajua kama tuna kazi kubwa katika mechi dhidi ya Msumbiji,”
alisema Canavaro ambaye pia ni nahodha wa Yanga.
Stars na Msumbiji zinatarajiwa kukutana Julai 20 mwaka huu,
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo timu hiyo, imerejea mwishoni mwa
wiki iliyopita ikitokea Botswana kwa kambi ya wiki mbili.
NA SALMA JUMA
No comments:
Post a Comment