Tuesday, February 3, 2015

JK afichua kipigo cha Lipumba

Na Fredy Azzah

SIKU chache baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na wafuasi wake kupigwa na polisi, Rais Jakaya Kikwete amesema tukio hilo limetokea kwa sababu nchi inaongozwa kwa sheria na atakayekiuka atakumbana na mkono wa sheria.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya mazungumzo ya faragha na mgeni wake, Rais wa Ujerumani, Joachim Gauck, ambaye yuko nchini kwa ziara ya siku tano.
Kabla ya Rais Kikwete kutoa kauli hiyo, Rais Gauck aliimwagia sifa Tanzania kutokana na namna inavyofuata utawala wa sheria, uhuru wa vyombo vya habari na kulinda haki za binadamu.
Baada ya viongozi hao kuzungumza mbele ya waandishi wa habari juu ya ziara hiyo, waandishi walipewa fursa ya kuuliza maswali na ndipo mmoja wa wanahabari kutoka Ujerumani, alipotaka kauli ya Rais Kikwete na Rais Gauck, juu ya msingi wa uhuru wa vyombo vya habari na haki za binadamu nchini, wakati hivi karibuni gazeti la The East African lilifungiwa na wanachama wa CUF kupigwa na polisi walipotaka kuandamana.
Akijibu swali hilo, Rais Kikwete alisema: “Tuna sheria zinazoongoza mambo hayo, huwezi kuamka tu ukaamua kuandamana, tuna taratibu zetu za vyama vya siasa kukusanyika, wala hatubani haki na uhuru wa wapinzani, ukivunja sheria hiyo utawajibishwa.
 “Na hapa wapinzani ndio wanafanya mikutano mingi kuliko chama tawala, ikitokea hawajafuata taratibu, hatuwezi kuwaacha waendelee kuvunja sheria,” alisema Rais Kikwete.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Profesa Lipumba alisema walifuata sheria zote na pia kutii amri ya polisi ya kuwataka kuacha kuandamana na kufanya mkutano wa hadhara.
CUF walipanga kuandamana na kufanya mkutano wa hadhara kukumbuka wenzao waliouawa mwaka 2001.
Kuhusu kufungiwa kwa gazeti la kila wiki la The East African linalochapishwa nchini Kenya na Kampuni ya Nation Media Group (NMG) na kusambazwa Tanzania, Rais Kikwete alisema halijafungiwa bali lilibainika kusambazwa nchini bila kuwa na kibali.
Alisema baada ya kubainika hilo, kampuni inayochapisha gazeti hilo ilitakiwa kutoendelea kulisambaza nchini hadi kibali cha kufanya hivyo kitakapopatikana.
Rais Kikwete alisema kwa sasa utaratibu wa kutoa kibali hicho unaendelea.
Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani ambazo zinajali uhuru wa vyombo vya habari, na hata sasa kuna magazeti mengi yaliyosajiliwa na yanachapishwa kila siku.
Akizungumzia kuhusu hali ya usalama na tishio la ugaidi, Rais Kikwete alisema hawezi kusema kuwa Tanzania iko salama asilimia 100, lakini kutokana na hatua zinazochukuliwa za kulinda amani na usalama, hali iko shwari.
“Tunashirikiana vizuri na vyombo vya usalama vya kimataifa, tunadabilishana taarifa kila inapobidi, siwezi kusema kuwa sisi tuko salama kwa asilimia 100, kwamba hatuwezi kuguswa kutokana na mikakati ya kulinda amani, hali kwetu ipo shwari,” alisema.
Katika hatua nyingine, aliiomba Ujerumani kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini, ikiwamo gesi, viwanda na biashara.
Alisema Tanzania baada ya kugundua gesi asilia, pamoja na mambo mengine itatumika kwa matumizi ya nyumbani kwani kwa sasa zaidi ya tani 40 za mkaa hutumika Dar es Salaam pekee kila mwaka, hivyo kiasi kikubwa cha miti huteketea.
Kwa upande wake, Rais Gauck, alisema Ujerumani iko tayari kuendeleza ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi na Tanzania na ndiyo maana katika msafara wake ameongozana na wadau mbalimbali wa sekta za kiuchumi, wakiwamo wafanyabiashara wakubwa na waziri husika kwa lengo la kujifunza na kuangalia fursa za uwekezaji.
Alisema anaridhishwa na jinsi Tanzania inavyosimamia haki za binadamu na kasi ya kushughulikia tatizo la rushwa, umoja wa kitaifa na maendeleo,
na kwamba Ujerumani itaendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za maendeleo na Tanzania.
Rais Gauck alisema nchi hizi mbili zimekuwa na ushirikiano wa kihistoria tangu mwaka 1961, na ndiyo maana kuna miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii iliyotekelezwa, na kwamba Ujerumani inaisaidia kiuchumi Tanzania.
Aliipongeza pia Tanzania kutokana na kushiriki katika kutuliza migogoro ya kikanda, ikiwa ni pamoja na kutafuta amani Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). 
Alisema Tanzania ni mfano wa kuigwa kwa jinsi inavyojituma kupeleka majeshi yake katika mataifa yenye machafuko, kwani kwa kufanya hivyo inajilinda yenyewe.
Rais Gauck anatarajiwa pia kutembelea Zanzibar, Bagamoyo, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na ameomba akae Arusha kwa muda kabla ya kurejea Ujerumani, kwani mji huo una sifa ya kipekee duniani.

Simba yafuata dawa Zanzibar

SAADA AKIDA NA SALMA MPELI

KOCHA wa Simba, Goran Kopunovic, ameziangalia silaha zote ndani ya kikosi chake kinachoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kuuomba uongozi umpe muda zaidi ajichimbie na timu kisiwani Zanzibar kwa ajili ya kukipika zaidi kikosi chake.

Goran anaonekana kunogewa na marashi ya Zanzibar yaliyompa ubingwa Kombe la Mapinduzi na ndiyo maana ameamua kukipeleka tena kikosi chake kisiwani humo kwa ajili ya maandalizi ya mechi za mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Simba imekuwa na desturi ya kujichimbia kisiwani humo, hasa inapokabiliwa na mechi ngumu pekee, ikiwemo ya mahasimu wa jadi kisoka, Yanga, lakini sasa Kopunovic amesema kambi ya Zanzibar ndiyo anaamini itampa ubingwa.
Mserbia huyo alianza kazi ya kuinoa Simba Januari Mosi, mwaka huu, kwenye michuano ya Mapinduzi na kuipa taji hilo, akisifia mazingira ya utulivu yalisaidia timu yake kufanya vema.
Habari za uhakika kutoka ndani ya uongozi wa Simba zinaeleza Kopunovic amependekeza timu yake kurejea visiwani Unguja baada ya kupaona ni sehemu tulivu kwake kuweza kuwajenga wachezaji kisaikolojia.
"Unajua kule ndipo alipoanzia kazi, kwani aliikuta timu katika michuano ya Mapinduzi ambapo ameyapenda mazingira ya kule akidai ni sehemu tulivu, hivyo ameuomba uongozi kuhakikisha unawafanyia mpango ili timu iweze kwenda tena kujichimbia huko," kilisema chanzo hicho.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, timu hiyo itakwenda kisiwani humo baada ya mchezo wao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union, utakaopigwa mwishoni mwa wiki hii katika Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.
DIMBA Jumatano lilimtafuta Ofisa Habari wa klabu hiyo, Humphrey Nyasio ili kuzungumzia suala hilo, ambapo hakukubali wala kukataa zaidi ya kusema akili yao yote ipo katika mchezo wao huo dhidi ya Coastal Union, kwani wanahitaji pointi zote tatu.
Akizungumzia kurejea kwa kipa wao namba mbili, Hussein Sharrif 'Cassilas', alisema mwishoni mwa wiki hii anatarajiwa kuungana na wenzake katika mazoezi mara baada ya kumaliza mchezo wao dhidi ya Coastal Union.
"Cassillas tunatarajia atajiunga na wenzake mwishoni mwa wiki hii baada ya kutoka Tanga, suala la beki wa kati, Joseph Owino bado anaendelea na matibabu, kwani aliumia nyonga," alisema Nyasio.

Baadhi ya wachezaji wa Simba wakiwa wanaingia uwanjani.

Yanga yatua kininja Tanga

NA EZEKIEL TENDWA
YANGA iko jijini Tanga ilikokwenda kuvaana na Coastal Union ya huko katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. Wanajangwani hao walitua Tanga 'kininja' tangu juzi, kabla ya kutoweka na kwenda mafichoni kukwepa hujuma za wapinzani wao wanaojulikana kwa jina la 'Wagosi wa Kaya'.
Timu hizo zinavaana leo katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa katika uwanja wa CCM Mkwakwani.
Kikosi cha timu hiyo kilitua Tanga juzi kwa mbwembwe nyingi na kupokewa kifalme na mashabiki wake, huku msafara wake ukiwa chini ya ulinzi mkali wa magari sita mbele na nyuma.
Msafara wa timu hiyo ulipelekwa moja kwa moja kwenye tawi la klabu hiyo katika mji mdogo  wa Pongwe, lililoko umbali wa kilomita 35 kutoka jijini Tanga.
Kwa kutambua inaweza kufanyiwa hujuma na wenyeji wao, Coastal Union, Yanga iliamua kukipeleka mafichoni kikosi katika Hoteli ya Central iliyoko katikati ya jiji hilo, huku makomandoo wa timu hiyo wakilazimika kuweka ulinzi wa kutosha kwa wageni wanaoingia na kutoka.
Itakumbukwa Yanga inacheza na Coastal Union ikiwa ni siku chache ikitoka kukipiga na Ndanda FC na kulazimishwa sare ya bila kufungana, matokeo yaliyowakasirisha mashabiki wa timu hiyo kuhisi pengine inahujumiwa na baadhi ya watu.
Mara baada ya taarifa za Yanga kutua jijini humo kuenea, baadhi ya wadau wa soka, wakiwemo wanazi wa timu hiyo walianza kuisaka kutaka kuwaona baadhi ya wachezaji nyota wa kimataifa kama Mliberia Kpah Sherman, Andrey Coutinho na Amis Tambwe, lakini wakashindwa kujua iliko.
Uchunguzi uliofanywa na DIMBA Jumatano ulibaini mashabiki hao walikuwa na hamu ya kuwaona wachezaji hao ambao Yanga iliwasajili msimu huu, kwani hawajawahi kuwaona isipokuwa Tambwe, ambaye msimu uliopita alikuwa Simba.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Yanga zilieleza uongozi wa klabu hiyo uliamua kufanya mambo yao kwa siri na kuficha uwanja walioutumia kwa mazoezi, ili kukwepa mtego wa  wapinzani wao, hali iliyowafanya mashabiki wa timu hiyo kuzidi kuhaha.
Kikosi cha timu hiyo kutokana na uchovu wa safari kilishindwa kufanya mazoezi ambapo benchi la ufundi liliamua programu ya mwisho ya kujifua ingeanza jana jioni kwenye uwanja wa Mkwakwani.
Huu ni mchezo wa kiporo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao unatarajiwa kuwa mkali kwa dakika zote 90, kwani kila timu inahitaji matokeo mazuri ili kujiweka kwenye mazingira mazuri, ikizingatiwa kuwa Ligi yenyewe imefikia patamu.
Yanga wapo nafasi ya pili wakiwa na pointi 19 nyuma ya mabingwa watetezi, Azam FC,waliopo kileleni wakiwa na pointi 21 na kama Wanajangwani hao wataibuka na ushindi watapanda juu na kuwazidi Wanalambalamba hao kwa pointi moja.
Kwa upande wao, Coastal Union wapo nafasi ya sita wakiwa na pointi 17 na kama nao wataibuka na ushindi watapanda hadi nafasi ya pili wakifikisha pointi 20 na kuwaacha nyuma Yanga kwa pointi moja, kitu ambacho kinaufanya mchezo huo kuwa wa shika nikushike.
Yanga chini ya Kocha wao Mkuu, Mholanzi Hans Van Pluijm, itawategemea zaidi mastraika wao mahiri, Tambwe, Sherman na Mrwanda mwenye mabao matano, akizidiwa kwa mabao mawili na Didier Kavumbagu wa Azam mwenye mabao saba na Rashid Mandwa wa Kagera Sugar na Samuel Kamuntu wa JKT Ruvu kila mmoja akiwa na mabao sita.
Hata hivyo, Yanga wasitarajie mteremko, kwani Coastal Union kupitia kwa Msemaji wao, Oscar Asenga, wameapa kula sahani moja na Wanajangwani hao, wakitaka kuhakikisha wanautumia vizuri uwanja wao wa nyumbani na kuibuka na ushindi ili dhamira yao ya kumaliza moja ya nafasi za juu msimu huu itimie.
"Kama watu wanadhani Yanga watakuwa na kazi rahisi wamekosea, hatuwezi kukubali kudondosha pointi tatu, tena kwenye uwanja wetu wa nyumbani, sisi tuna pointi 17 kama tukiwashinda tutakuwa nafasi ya pili kwa kufikisha pointi 20, vijana wetu wanajua nini tunakitafuta msimu huu," alisema Asenga.
Takwimu zinaonyesha mara ya mwisho Yanga kuifunga Coastal Union ilikuwa ni Novemba 11, 2012, kwenye uwanja wa Mkwakwani, ikishinda 2-0 lakini baada ya hapo timu hizo zimekuwa zikienda sare katika mechi zote zilizofuata.
Mei 18, 2013, timu hizo zilikutana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kwenda sare ya bao 1-1 na kukutana tena Agosti 28, 2014, kwenye uwanja huo na kutoka sare nyingine kama hiyo.
Aidha mechi ya mwisho kuzikutanisha timu hizo ilikuwa ni ile ya Januari 29, mwaka jana jijini Tanga, ambapo timu hizo zilitoka suluhu pia.

 Kikosi cha Yanga kikiwa mazoezini.