Na Fredy Azzah
SIKU chache
baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na
wafuasi wake kupigwa na polisi, Rais Jakaya Kikwete amesema tukio hilo
limetokea kwa sababu nchi inaongozwa kwa sheria na atakayekiuka atakumbana na
mkono wa sheria.
Rais Kikwete alitoa
kauli hiyo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na waandishi
wa habari baada ya kufanya mazungumzo ya faragha na mgeni wake, Rais wa Ujerumani,
Joachim Gauck, ambaye yuko nchini kwa ziara ya siku tano.
Kabla ya Rais
Kikwete kutoa kauli hiyo, Rais Gauck aliimwagia sifa Tanzania kutokana na namna
inavyofuata utawala wa sheria, uhuru wa vyombo vya habari na kulinda haki za
binadamu.
Baada ya
viongozi hao kuzungumza mbele ya waandishi wa habari juu ya ziara hiyo,
waandishi walipewa fursa ya kuuliza maswali na ndipo mmoja wa wanahabari kutoka
Ujerumani, alipotaka kauli ya Rais Kikwete na Rais Gauck, juu ya msingi wa uhuru
wa vyombo vya habari na haki za binadamu nchini, wakati hivi karibuni gazeti la
The East African lilifungiwa na wanachama wa CUF kupigwa na polisi walipotaka
kuandamana.
Akijibu swali
hilo, Rais Kikwete alisema: “Tuna sheria zinazoongoza mambo hayo, huwezi kuamka
tu ukaamua kuandamana, tuna taratibu zetu za vyama vya siasa kukusanyika, wala
hatubani haki na uhuru wa wapinzani, ukivunja sheria hiyo utawajibishwa.
“Na hapa wapinzani ndio wanafanya mikutano
mingi kuliko chama tawala, ikitokea hawajafuata taratibu, hatuwezi kuwaacha
waendelee kuvunja sheria,” alisema Rais Kikwete.
Akizungumza na
waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Profesa Lipumba alisema walifuata sheria
zote na pia kutii amri ya polisi ya kuwataka kuacha kuandamana na kufanya
mkutano wa hadhara.
CUF walipanga kuandamana
na kufanya mkutano wa hadhara kukumbuka wenzao waliouawa mwaka 2001.
Kuhusu kufungiwa
kwa gazeti la kila wiki la The East African linalochapishwa nchini Kenya na
Kampuni ya Nation Media Group (NMG) na kusambazwa Tanzania, Rais Kikwete
alisema halijafungiwa bali lilibainika kusambazwa nchini bila kuwa na kibali.
Alisema baada ya
kubainika hilo, kampuni inayochapisha gazeti hilo ilitakiwa kutoendelea
kulisambaza nchini hadi kibali cha kufanya hivyo kitakapopatikana.
Rais Kikwete alisema
kwa sasa utaratibu wa kutoa kibali hicho unaendelea.
Alisema Tanzania
ni miongoni mwa nchi chache duniani ambazo zinajali uhuru wa vyombo vya habari,
na hata sasa kuna magazeti mengi yaliyosajiliwa na yanachapishwa kila siku.
Akizungumzia kuhusu
hali ya usalama na tishio la ugaidi, Rais Kikwete alisema hawezi kusema kuwa
Tanzania iko salama asilimia 100, lakini kutokana na hatua zinazochukuliwa za
kulinda amani na usalama, hali iko shwari.
“Tunashirikiana
vizuri na vyombo vya usalama vya kimataifa, tunadabilishana taarifa kila
inapobidi, siwezi kusema kuwa sisi tuko salama kwa asilimia 100, kwamba
hatuwezi kuguswa kutokana na mikakati ya kulinda amani, hali kwetu ipo shwari,”
alisema.
Katika hatua
nyingine, aliiomba Ujerumani kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini, ikiwamo
gesi, viwanda na biashara.
Alisema Tanzania
baada ya kugundua gesi asilia, pamoja na mambo mengine itatumika kwa matumizi
ya nyumbani kwani kwa sasa zaidi ya tani 40 za mkaa hutumika Dar es Salaam
pekee kila mwaka, hivyo kiasi kikubwa cha miti huteketea.
Kwa upande wake,
Rais Gauck, alisema Ujerumani iko tayari kuendeleza ushirikiano wa kisiasa na
kiuchumi na Tanzania na ndiyo maana katika msafara wake ameongozana na wadau
mbalimbali wa sekta za kiuchumi, wakiwamo wafanyabiashara wakubwa na waziri
husika kwa lengo la kujifunza na kuangalia fursa za uwekezaji.
Alisema anaridhishwa
na jinsi Tanzania inavyosimamia haki za binadamu na kasi ya kushughulikia
tatizo la rushwa, umoja wa kitaifa na maendeleo,
na kwamba
Ujerumani itaendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za
maendeleo na Tanzania.
Rais Gauck alisema
nchi hizi mbili zimekuwa na ushirikiano wa kihistoria tangu mwaka 1961, na
ndiyo maana kuna miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii iliyotekelezwa, na
kwamba Ujerumani inaisaidia kiuchumi Tanzania.
Aliipongeza pia
Tanzania kutokana na kushiriki katika kutuliza migogoro ya kikanda, ikiwa ni
pamoja na kutafuta amani Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Alisema Tanzania
ni mfano wa kuigwa kwa jinsi inavyojituma kupeleka majeshi yake katika mataifa
yenye machafuko, kwani kwa kufanya hivyo inajilinda yenyewe.
Rais Gauck
anatarajiwa pia kutembelea Zanzibar, Bagamoyo, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na
ameomba akae Arusha kwa muda kabla ya kurejea Ujerumani, kwani mji huo una sifa
ya kipekee duniani.
No comments:
Post a Comment