Yanga yatua kininja Tanga
NA EZEKIEL TENDWA
YANGA iko jijini Tanga ilikokwenda kuvaana na Coastal Union ya huko katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. Wanajangwani hao walitua Tanga 'kininja' tangu juzi, kabla ya kutoweka na kwenda mafichoni kukwepa hujuma za wapinzani wao wanaojulikana kwa jina la 'Wagosi wa Kaya'.
Timu hizo zinavaana leo katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa katika uwanja wa CCM Mkwakwani.
Kikosi cha timu hiyo kilitua Tanga juzi kwa mbwembwe nyingi na kupokewa kifalme na mashabiki wake, huku msafara wake ukiwa chini ya ulinzi mkali wa magari sita mbele na nyuma.
Msafara wa timu hiyo ulipelekwa moja kwa moja kwenye tawi la klabu hiyo katika mji mdogo wa Pongwe, lililoko umbali wa kilomita 35 kutoka jijini Tanga.
Kwa kutambua inaweza kufanyiwa hujuma na wenyeji wao, Coastal Union, Yanga iliamua kukipeleka mafichoni kikosi katika Hoteli ya Central iliyoko katikati ya jiji hilo, huku makomandoo wa timu hiyo wakilazimika kuweka ulinzi wa kutosha kwa wageni wanaoingia na kutoka.
Itakumbukwa Yanga inacheza na Coastal Union ikiwa ni siku chache ikitoka kukipiga na Ndanda FC na kulazimishwa sare ya bila kufungana, matokeo yaliyowakasirisha mashabiki wa timu hiyo kuhisi pengine inahujumiwa na baadhi ya watu.
Mara baada ya taarifa za Yanga kutua jijini humo kuenea, baadhi ya wadau wa soka, wakiwemo wanazi wa timu hiyo walianza kuisaka kutaka kuwaona baadhi ya wachezaji nyota wa kimataifa kama Mliberia Kpah Sherman, Andrey Coutinho na Amis Tambwe, lakini wakashindwa kujua iliko.
Uchunguzi uliofanywa na DIMBA Jumatano ulibaini mashabiki hao walikuwa na hamu ya kuwaona wachezaji hao ambao Yanga iliwasajili msimu huu, kwani hawajawahi kuwaona isipokuwa Tambwe, ambaye msimu uliopita alikuwa Simba.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Yanga zilieleza uongozi wa klabu hiyo uliamua kufanya mambo yao kwa siri na kuficha uwanja walioutumia kwa mazoezi, ili kukwepa mtego wa wapinzani wao, hali iliyowafanya mashabiki wa timu hiyo kuzidi kuhaha.
Kikosi cha timu hiyo kutokana na uchovu wa safari kilishindwa kufanya mazoezi ambapo benchi la ufundi liliamua programu ya mwisho ya kujifua ingeanza jana jioni kwenye uwanja wa Mkwakwani.
Huu ni mchezo wa kiporo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao unatarajiwa kuwa mkali kwa dakika zote 90, kwani kila timu inahitaji matokeo mazuri ili kujiweka kwenye mazingira mazuri, ikizingatiwa kuwa Ligi yenyewe imefikia patamu.
Yanga wapo nafasi ya pili wakiwa na pointi 19 nyuma ya mabingwa watetezi, Azam FC,waliopo kileleni wakiwa na pointi 21 na kama Wanajangwani hao wataibuka na ushindi watapanda juu na kuwazidi Wanalambalamba hao kwa pointi moja.
Kwa upande wao, Coastal Union wapo nafasi ya sita wakiwa na pointi 17 na kama nao wataibuka na ushindi watapanda hadi nafasi ya pili wakifikisha pointi 20 na kuwaacha nyuma Yanga kwa pointi moja, kitu ambacho kinaufanya mchezo huo kuwa wa shika nikushike.
Yanga chini ya Kocha wao Mkuu, Mholanzi Hans Van Pluijm, itawategemea zaidi mastraika wao mahiri, Tambwe, Sherman na Mrwanda mwenye mabao matano, akizidiwa kwa mabao mawili na Didier Kavumbagu wa Azam mwenye mabao saba na Rashid Mandwa wa Kagera Sugar na Samuel Kamuntu wa JKT Ruvu kila mmoja akiwa na mabao sita.
Hata hivyo, Yanga wasitarajie mteremko, kwani Coastal Union kupitia kwa Msemaji wao, Oscar Asenga, wameapa kula sahani moja na Wanajangwani hao, wakitaka kuhakikisha wanautumia vizuri uwanja wao wa nyumbani na kuibuka na ushindi ili dhamira yao ya kumaliza moja ya nafasi za juu msimu huu itimie.
"Kama watu wanadhani Yanga watakuwa na kazi rahisi wamekosea, hatuwezi kukubali kudondosha pointi tatu, tena kwenye uwanja wetu wa nyumbani, sisi tuna pointi 17 kama tukiwashinda tutakuwa nafasi ya pili kwa kufikisha pointi 20, vijana wetu wanajua nini tunakitafuta msimu huu," alisema Asenga.
Takwimu zinaonyesha mara ya mwisho Yanga kuifunga Coastal Union ilikuwa ni Novemba 11, 2012, kwenye uwanja wa Mkwakwani, ikishinda 2-0 lakini baada ya hapo timu hizo zimekuwa zikienda sare katika mechi zote zilizofuata.
Mei 18, 2013, timu hizo zilikutana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kwenda sare ya bao 1-1 na kukutana tena Agosti 28, 2014, kwenye uwanja huo na kutoka sare nyingine kama hiyo.
Aidha mechi ya mwisho kuzikutanisha timu hizo ilikuwa ni ile ya Januari 29, mwaka jana jijini Tanga, ambapo timu hizo zilitoka suluhu pia.
Kikosi cha Yanga kikiwa mazoezini.
No comments:
Post a Comment