NA MWANDISHI WETU
KOCHA Mkuu wa Simba, Goran Kopunovic, ameamua kubadili kikosi chake ili aweze kuifanyia kitu mbaya Azam FC katika mchezo utakaozikutanisha timu hizo wikiendi hii kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Simba na Azam zitapambana Jumapili kuwania kuweka sawa mipango ya kushika nafasi ya pili, ili kupata tiketi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
Azam wapo nafasi ya pili wakiwa na pointi 45, Simba wakiwa nyuma yao katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 41, wakibakiwa na michezo miwili, huku wakiwaombea mabaya Wanalambalamba hao wapoteze michezo yao mitatu ili wawapiku.
Kama Simba watashinda michezo yao hiyo miwili dhidi ya Azam na JKT Ruvu na Wanalambalamba hao wakafanya vibaya michezo yao, ikiwamo huo wa Simba, Yanga pamoja na Mgambo JKT itawapa fursa ya kumaliza nafasi ya pili.
Kutokana na hali hiyo, Kocha Mkuu wa Simba, Goran Kopunovic, ameanza kuzichanga vema karata zake ili kuhakikisha anawashushia kipigo Azam FC na baadaye kumalizia kwa maafande wa JKT Ruvu.
Akizungumza na DIMBA Jumatano, Kopunovic alisema, anaangalia uwezekano wa kubadili kikosi chake kwa namna ambavyo anajua yeye, ili kuwachanganya wapinzani wake na kupata kile ambacho amekikusudia.
"Kila kitu kinakwenda vizuri, naamini kwa jinsi nitakavyokipanga kikosi changu tutafikia malengo yetu, kilichopo ni kila Mwanasimba kujitolea kwa hali yoyote," alisema.
No comments:
Post a Comment