Wednesday, April 29, 2015

Ngassa afichua siri ya ubingwa Jangwani

NA ZAINAB IDDY
WINGA wa kutegemewa wa mabingwa wapya wa Ligi Kuu Tanzania Bara (Yanga), Mrisho Khalfani Ngassa 'Anko,' amefichua siri ya timu hiyo kutwaa ubingwa msimu huu kuwa ni uwepo wa benchi la ufundi lenye weledi wa soka.
Yanga juzi iliweza kutangaza ubingwa baada ya kuifunga Polisi Morogoro mabao 4-1 na kufikisha jumla ya pointi 55, ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote hata mabingwa wa msimu uliopita, Azam FC waliopo nafasi ya pili na pointi 45 katika msimamo wa ligi hiyo.
Ngassa ameliambia DIMBA Jumatano kuwa mafanikio ya kikosi chao yanatokana na ujuzi wa makocha wao.
Ngassa alisema pongezi nyingi zinastahili kwenda kwa makocha Hans  van der Pluijm  pamoja na msaidizi wake, Charles Mkwassa, ambao wameweza kuwaweka wachezaji kuwa kitu kimoja na hamasa wanazozitoa pindi kikosi kinapopata matokeo mazuri  au mabaya ndizo zilizochangia kujituma kwa kila mmoja wao.
Alisema licha ya mchezaji mmoja mmoja kujitengenezea jina katika soka la Tanzania, lakini  kocha ndiye nguzo muhimu kwao katika kuhakikisha matokeo bora yanapatikana.
"Kama inavyokuwa timu ikifanya vibaya mzigo wa lawama wanabebeshwa makocha, basi hata ubingwa wetu msimu huu wao ndiyo wanastahili pongezi nyingi kutokana na jitihada zao binafsi za kutumia akili za ziada ili kuhakikisha kikosi kinakuwa cha ushindani pasipo kujali changamoto za ligi yenyewe.
"Walihakikisha tunakuwa kitu kimoja, tunajituma kila mmoja kwa nafasi yake, huku  wakipigania kuona tunapata kila kinachohitajika kwa mchezaji ili aweze kufanya kazi yake kwa moyo mmoja, hizo ni juhudi kubwa ambazo si makocha wote wanaweza kuzifanya,"  alisema.
Hadi sasa Yanga imefanikiwa kutwaa kombe la Ligi Kuu Tanzania Bara mara 25 na kushikilia rekodi ya kuwa mabingwa mara nyingi zaidi, wakifuatiwa na Simba waliolinyakua mara 19.

No comments:

Post a Comment