Wednesday, April 29, 2015

Tambwe aweka rekodi ya kutisha Ligi Kuu

Na Mwandishi Wetu
STRAIKA wa Yanga, raia wa Burundi, Amissi Tambwe, ameweka bonge la rekodi ya kutisha kwa kuwa mchezaji wa kwanza kupiga hat-trick (mabao matatu mechi moja) ya pili msimu huu, ikiwa ni ya nne kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Mrundi huyo ni mchezaji pekee aliyeweka rekodi hiyo ambayo haijawahi kuwekwa na mchezaji yeyote tangu uwanja huo ulipoanza kutumika.
Mechi ya kwanza kwa straika huyo kufunga hat trick kwenye uwanja huo ilikuwa ni Februari Mosi, 2014, dhidi ya JKT Oljoro, akiwa na Simba, ambayo ilishinda 4-0.
Mechi nyingine ambayo Mrundi huyo alifunga hat trick ilikuwa ni Septemba 19, 2014 dhidi ya Mgambo JKT, ambayo timu yake ya Simba ilipata ushindi mnono wa mabao 6-0.
Mshambuliaji huyo alikamilisha rekodi yake ya kupiga hat-trick ya tatu Aprili 8, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, kwa kufunga mabao manne katika ushindi wa mabao 8-0 dhidi ya Coastal Union, iliyocheza na Yanga.

Tambwe, aliyekuwa mfungaji bora msimu uliopita wa ligi kuu, akifunga mabao 19, alitua kuichezea Yanga kwenye usajili wa dirisha dogo msimu huu akitokea Simba, baada ya kumsitishia mkataba wake kabla ya kutua Jangwani.
Upo uwezekano mkubwa wa mshambuliaji huyo kukitetea kiatu chake cha dhahabu kutokana na kasi yake kubwa aliyonayo hivi sasa ya kufunga mabao.
Mrundi huyo, hadi hivi sasa amefanikiwa kufunga mabao 14, akiongozwa na Simon Msuva mwenye 17, akifuatiwa na mshambuliaji wa Azam FC, Didier Kavumbagu aliyepachika 10 na Rashid Mandawa wa Kagera Sugar ambaye naye ana mabao 10.
Kati ya hat-trick hizo alizozipiga, idadi kubwa ya mabao amefunga kwa kichwa, kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufunga aina hiyo ya mabao, huku mengine akifunga kwa kumchambua kipa.

No comments:

Post a Comment