Wednesday, April 22, 2015

Mechi nne kuondoka na watu Simba


NA EZEKIEL TENDWA
WAKATI Simba ikiwa imebakisha michezo minne ikianzia na wa leo dhidi ya Mgambo JKT kumaliza Ligi  Kuu Tanzania Bara, wachezaji wa timu hiyo watacheza kwa tahadhari kubwa kuepuka panga la usajili mara Ligi hiyo itakapofikia tamati Mei, mwaka huu.
Simba wapo nafasi ya tatu wakiwa na pointi zao 35, nyuma ya Azam wenye pointi 42, kila timu ikiwa imecheza michezo 22, zikibakiwa na michezo minne kumalizia Ligi hiyo ambapo kila moja ikiapa kushinda michezo yake yote.
Ili Simba wamalize nafasi ya pili, wanatakiwa washinde michezo yao yote minne iliyobaki, ukiwamo dhidi ya Azam FC, huku wakiwaombea Wanalambalamba hao kupoteza angalau michezi mitatu kati ya minne waliyobakiwa nayo.
Kocha Mkuu wa Simba, Goran Kopunovic, ameweka wazi kuwa bado ana matumaini ya kikosi chake kumaliza katika nafasi ya pili, huku akitamba kuibuka na ushindi mnono dhidi ya maafande hao wa Mgambo leo, ili kuzidi kuwasogelea Azam.
Ukiacha mchezo wa leo, Simba imesaliwa na mechi dhidi ya Azam FC, Ndanda FC na  JKT Ruvu.
Michezo yote hiyo Simba wataicheza katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, huku wapenzi na mashabiki wao wakiwa na hamu ya kuona kikosi hicho kinashinda michezo hiyo ili kujiweka katika mazingira ya kupata nafasi ya kucheza michuano ya kimataifa mwakani, huku wakiwaombea mabaya Azam FC.
Habari za uhakika ambazo Dimba Jumatano inazo ni kwamba, baadhi ya wachezaji ambao wamesajiliwa kwa bei kubwa na kushindwa kuonyesha cheche zao wapo kwenye wakati mgumu wa kama wataendelea kuwepo kwenye kikosi hicho msimu ujao au kutemwa.
Wachezaji wa Kimataifa, Danny Sserunkuma pamoja na Simon Sserunkuma wapo kwenye mtihani mgumu, kutokana na kusajiliwa kwa bei kubwa huku wakishindwa kufanya mambo ya kulikuna benchi la ufundi.


No comments:

Post a Comment