Wednesday, April 22, 2015

Nyota ya Ngassa yazidi kung’aa Afrika


NA SHARIFA MMASI
WAKATI winga wa Yanga, Mrisho Ngassa akiwa amemaliza mkataba wake ndani ya kikosi hicho, nyota yake imezidi kung’aa barani Afrika, baada ya klabu kadhaa kuonyesha kukunwa na kiwango chake, hivyo kuitaka saini yake kwa udi na uvumba.
Awali Ngassa alishafanya mazungumzo na kusaini mkataba wa awali na timu ya Free State ya Afrika Kusini, lakini moja ya timu kubwa ya nchini Qatar pia imeonyesha nia ya kumhitaji kabla ya Etoile du Sahel ya Tunisia nayo kufunguka juu ya mchezaji huyo.
Habari za uhakika ambazo DIMBA Jumatano imezipata zinaeleza kuwa, mbali na timu hizo, pia klabu ya AS Vita ya Congo  DRC nayo inahitaji saini ya winga huyo, huku klabu yake, Yanga nao wakihaha kumshawishi kumpa mkataba mpya baada ya kuwafanyia mambo kwenye Ligi Kuu na michuano ya kimataifa.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro, amekiri Ngassa kumaliza mkataba wake na klabu hiyo na kusema suala la mchezaji huyo kutamaniwa na timu mbalimbali barani Afrika kwa sasa halina nafasi kwao, kwani kila kitu kitawekwa wazi baada ya ligi kumalizika Mei, mwaka huu.
"Ni kweli kwamba Ngassa amemaliza mkataba wake, lakini kama mnavyomwona anaendelea kuichezea Yanga hivyo tunawaomba mashabiki wetu wala wasiwe na wasiwasi juu ya jambo hilo, kwani uongozi wao upo makini," alisema Muro.


No comments:

Post a Comment