Wednesday, March 30, 2016

African Sports kusaka kocha Zanzibar

NA SALMA MPELI
UONGOZI wa African Sports ya Tanga upo katika harakati ya kumsaka kocha kutoka visiwani Zanzibar atakayeziba nafasi ya Ramadhan Aluko aliyefukuzwa hivi karibuni.
Akizungumza na DIMBA, Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, Abdul Bosnia, alisema wanahitaji kocha kwa haraka na tayari wapo katika mchakato huo kwa ajili ya kuanza kazi mapema ili kuinusuru timu kutoka kwenye hatari ya kushuka daraja.
“Tunahitaji kocha kwa haraka baada ya kuamua kuachana na Aluko, tumelenga kutafuta mwalimu kutoka Unguja ili aanze kazi mapema,” alisema.
African Sports ipo nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na jumla ya pointi 20 juu ya ndugu zao Coastal Union ambao wanaburuza mkia wakiwa na pointi 19 ambapo timu hizo zote zipo kwenye hatari ya kushuka daraja.
Timu hiyo ilipanda daraja msimu uliopita na kuanza kucheza Ligi Kuu msimu huu baada ya kucheza ligi hiyo kwa mara ya mwisho mwaka 1988, lakini hata hivyo mashabiki wao wana wasiwasi mkubwa kutokana na majaliwa na timu hiyo katika msimu ujao wa ligi kwani huenda isiwepo msimu ujao.


No comments:

Post a Comment