Tuesday, October 28, 2014

Usemavyo ubongo wa Kakore




Hawa wametolewa kafara, tatizo lipo Simba
HIVI karibuni klabu ya Simba ilitangaza kuwasimamisha wachezaji wake watatu kwenye kikosi hicho ambao ni Haruna Chanongo, Shaaban Kisiga na Amri Kiemba kwa kile kilichoelezwa kuwa ni utovu wa nidhamu.
Lakini hapa najiuliza maswali mengi kuwa ni kweli tatizo la Simba ni Kiemba, Kisiga na Chanongo, Kocha Patrick Phiri na wasaidizi wake? Au kuna matatizo mengine makubwa zaidi ya haya tunayoyaona yakitokea sasa.
Lakini majibu ni mepesi ambayo hayahitaji hata elimu ya darasa la saba kujua ukweli wa mambo kwamba tatizo la Simba ni kubwa zaidi ya Kiemba na wenzake ambao mimi naamini kuwa wametolewa kafara huku matatizo ya msingi yakiachwa.
Ukiangalia Simba ilivyo sasa ina mpasuko na mgogoro uliotokana na makovu ya uchaguzi ambayo yalipelekea wanachama zaidi ya 60 kufukuzwa uanachama wao kwa kosa la kufungua kesi mahakamani wakati wa uchaguzi uliofanyika yapata siku 100 zilizopita.
Hii ni moja ya sababu kubwa ambayo inaifanya Simba ipepesuke kwenye ligi kwani ukweli uliopo ni kwamba kama klabu ikiwa haina umoja na amani ni ngumu kupata matokeo bora, jambo hili ndilo linaikumba Simba kwa sasa hivyo kuwaondoa kikosini wachezaji hawa ni tatizo lingine linaloendelea kutengenezwa katika timu badala ya kutatua.
Naamini kwamba, baada ya kuwafukuza au kuwaondoa kikosini Kiemba na wenzake, bado ndani ya timu hapawezi kuwa na utulivu kwani wapo wachezaji ambao wanaweza kucheza kwa hofu kwa kuamini kuwa nao wanaweza kufukuzwa jambo ambalo litawafanya kucheza chini ya kiwango.
Lakini jambo la pili ni kukosekana kwa mshikamano na sauti moja ambayo inaifanya Simba kuwa moja kama ambavyo kauli mbiu yake inavyosema ‘Nguvu Moja’, hii ni kutokana na mpasuko ambao niliueleza hapo awali.
Kwa maana hiyo ili kuwa na Simba imara, ni lazima kuhakikisha inawarejesha Wanasimba kwenye nyumba moja kwa njia ya kukusanya makundi yote na kuwa kwenye njia rahisi ya kuelekea kwenye mafanikio.
Juu ya jambo hili lazima uongozi wa Simba ukae na kufikiria namna bora ya kufanya ili Simba kuwa moja vinginevyo hayawezi kupatikana matokeo bora ndani ya timu hiyo kwa wakati huu. Nakumbuka nilishasema miezi kadhaa iliyopita kuwa suala la mpasuko na mgogoro ndani ya Simba linaweza kusababisha matatizo makubwa kwa wakati huo na wakati ujao ambao ndiyo haya tunayoyaona sasa.
Jambo la tatu ambalo ni miongoni mwa mambo nyeti ni ukosefu wa stamina kikosini, ambapo timu imekuwa ikichoka mapema ndiyo maana yenyewe imekuwa ikicheza muda wa dakika 45-60 pekee hivyo zinazobakia wapinzani wao wanakuwa wakimiliki mpira.
Kwa hali hiyo imefanya hata kama Simba inapata ushindi lakini inakwama kuulinda ushindi huo na matokeo yake kuruhusu mabao rahisi na wakati mwingine ni tofauti na jinsi ilivyopata mabao yake.
Haya ni mambo ambayo Simba inastahili kuyaangalia na kuyatolea maamuzi wakati huu kutokana na unyeti wake kwani tatizo la kiufundi linaonekana ingawa naamini linatokana na mambo nje ya dawati la ufundi.
Ninachokifahamu ni kwamba, iwapo Simba inahitaji matokeo bora ni lazima iangalie katika nyanja mbalimbali na si kuwafukuza wachezaji au kumfukuza kocha kwani naye taarifa zilizopo ni kwamba amepewa mechi tatu akishindwa kufanikiwa safari itakuwa imemkuta.
Ila naamini kocha akishafukuzwa wapo viongozi nao wanastahili kujiuzulu kwa manufaa ya klabu kwasababu kama wameshindwa kuongoza ni vizuri wakaachia Wanasimba wengine waweze kuongoza kwani huenda wakawa na mbinu mbadala za kuifanya Simba kupata ushindi.
Kwa mfano katika mchezo baina ya Simba na Caostal Union kwenye Uwanja wa Taifa, Simba ilitangulia kufunga lakini ikashindwa kuulinda ushindi wake na kujikuta inaambulia sare, mwenendo ambao umekuwa ukiendelea hivyo hivyo hadi sasa.
Ndiyo maana nasema kuwa tatizo la Simba si Kisiga, Chanongo wala Kiemba ila kuna matatizo mengine mengi ndani ya timu ambayo yameifanya Simba kushindwa kuwa bora ambapo moja ya sababu hizo ni kuwepo kwa mgawanyiko miongoni mwa wachezaji.
Kwa sasa ndani ya timu moja kuna wachezaji ambao wanaonekana ni bora na muhimu kuliko wengine, jambo hilo nalo linatajwa kuchangia Simba kushindwa kufanya vizuri hivyo lazima uongozi uchukue hatua ya kurekebisha matatizo hayo badala ya uamuzi wa huwatuhumu wachezaji hawa wanaijuhumu timu.
Kwa sasa Simba ipo katika nafasi ya 10 baada ya kucheza mechi tano, ikitoa sare mechi tano, ikifungwa mabao matano na ikiwa na pointi tano, lakini hadi sasa haijafungwa takwimu ambazo mimi naamini si mbaya ila nafasi iliyopo ndiyo mbaya ingawa kama matatizo niliyoyataja yakirekebishwa, inaweza kuisaidia timu hiyo kufanikiwa.
Mazingira ya sasa yanastahili kufanyiwa maamuzi ya busara ili kufanikiwa vinginevyo uongozi unaweza kuingia kwenye historia mbaya ya timu kushuka daraja ikiwa mikononi mwao jambo ambalo litakuwa ni la aibu ya mwaka ambayo haijaweza kumkuta kiongozi yeyote kwenye klabu hiyo kwa zaidi ya miaka 70.

Dogo Aslay: Siku ya Msanii imetupa heshima




NA MWANDISHI WETU

KIONGOZI wa kundi chipukizi la muziki wa dansi nchini, Yamoto Band, Dogo Aslay, amefunguka kuwa ushiriki wao kwenye tamasha la 'Siku ya Msanii' umeijengea heshima bendi hiyo.
Aslay ameliambia DIMBA Jumatano kwamba, tamasha hilo lilikuwa na sura ya kitaifa hivyo kupata kwao nafasi ya kutumbuiza kutawasaidia kuongeza mashabiki na kuheshimika kama ilivyo kwa bendi kongwe za muziki wa dansi nchini.
"Kwetu tunawapigia saluti waandaji wa siku ya msanii kutuchaguza kuwa watumbuizaji kwani Tanzania kuna bendi nyingi lakini tukawa pekee kupata nafasi hiyo.
Katika tamasha hilo wasanii Edward Said Tingatinga alitunukiwa tuzo ya Msanii aliyejitolea maisha yake yote katika maendeleo ya sanaa (Lifetime achievement award) na Josephat Kanuti kutoka Morogoro, ambaye alitunukiwa tuzo ya msanii aliyetoa mchango mkubwa katika jamii kupitia sanaa (Humanitarian award).
Siku ya Msanii Tanzania, iliandaliwa na kampuni ya Haak Neel Production na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na kudhaminiwa na Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, wachapishaji wa magazeti ya Bingwa, Dimba, Rai, Mtanzania na The African, Azam Media, Hugo Domingo, EFM, Mfuko wa Pensheni wa PSPF, Channel Ten na Magic FM.

Phiri apata nguvu mpya



NA JIMMY CHIKA
KOCHA wa Simba Mzambia, Patrick Phiri amefumba macho baada ya uongozi wa klabu hiyo kuwapiga chini nyota watatu wa timu hiyo, akapiga ngumi kifuani na kusema kikosi chake sasa kitazaliwa upya.
Phiri amesema uamuzi huo umerudisha ari yake ya kukinoa kikosi hicho kwani kabla ya hapo alionekana kukata tamaa.
Jana kocha huyo alikataa kufafanua juu ya tishio la Kamati ya Utendaji ya Simba iliyoketi mkoani Iringa na kutoa maamuzi ya kuwatimua wachezaji wake watatu, Shaaban Kisiga, Haruna Chonongo na Amri Kiemba, lakini akasema mabadiliko yaliyofanyika anaamini yataleta taswira mpya.
Akizungumza na gazeti hili, Phiri alisema yeye kama kocha aliwaambia viongozi wakae na kuangalia tatizo liko wapi na walirekebishe kwa hiyo anaamini kama waliona tatizo liko kwa wachezaji hao basi  wametekeleza maagizo yake.
Hata hivyo, mabadiliko hayo hayakupokewa vizuri na mashabiki wa Simba ambapo jana baadhi yao walivamia makao ya klabu hiyo na kuendesha vikao visivyo rasmi kupinga hatua hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mashabiki hao walisema, kinachoigharimu Simba kwa sasa ni hali ya kutokuwepo kwa uhusiano mzuri baina yao na kamwe si wachezaji.
Mashabiki hao wamewatetea wachezaji hao ambao wote hucheza nafasi ya kiungo, kuwa watahitajika sana katika mechi zijazo hasa kutokana na uzoefu wao.
Kiemba ambaye ndiye pekee aliyeongelea suala la kutimuliwa kwao, alisisitiza kwamba amepoteza ari ya kuitumikia timu hiyo kufuatia kitendo hicho alichokiita ni udhalilishaji kwake.
Rais wa klabu hiyo, Evance Aveva alitaja sababu ya kutimuliwa Kiemba kuwa ni kushuka kiwango, huku Kisiga na Chonongo wakituhumiwa kwa utovu wa nidhamu.
Hata hivyo, Aveva aliliambia DIMBA kwamba, wachezaji hao bado wako chini ya klabu hiyo hadi pale kikao cha kuwajadili kitakapofanyika keshokutwa Ijumaa na kutoa maamuzi ya pamoja.
Wakati hali ikiwa hivyo, uongozi wa Simba umempa Phiri mechi mbili zijazo za kushinda, dhidi ya Mtibwa Sugar Jumamosi hii na Ruvu Shooting wiki ijayo, vinginevyo utavunja mkataba wake.
Phiri amepewa mechi hizo ili kuinasua timu hiyo kutoka dimbwi la sare ambalo limeiandama timu hiyo tangu kuanza kwa ligi.
Katibu Mkuu wa Simba, Stephen Ally aliwaambia waandishi wa habari jana makao makuu ya klabu hiyo Mtaa wa Msimbazi kuwa, Phiri anaweza kuondolewa baada ya mechi hizo mbili iwapo matokeo hayatakuwa mazuri.
Ally amesema kwamba, sababu ya Kamati ya Utendaji kufikia maamuzi hayo ni kwamba, wakati anaajiriwa Agosti mwaka huu, Phiri alipewa kila alichokihitaji ili kujenga timu.
"Alitaka kambi ya Zanzibar akapewa, akataka mechi za majaribio akapatiwa na timu imeendelea kuwa kambini muda wote wa mashindano, ikiwemo ya Afrika Kusini," alisema Ally.
Phiri alifanya vizuri katika mechi za kirafiki, lakini baada ya kuanza kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzaia Bara ametoa sare mechi zote tano na Jumamosi wiki hii atakuwa Uwanja wa Jamhuri dhidi ya vinara, Mtibwa Sugar.
Aidha, Katibu huyo amesema kwamba wachezaji watatu waliosimamishwa, Kisiga, Amri Kiemba na Haroun Chanongo watakutana na Kamati ya Nidhamu Ijumaa kujibu tuhuma zao.
Katika hatua nyingine mechi ya Simba na Mtibwa inazidi kuwa katika mazingira magumu kwa timu hiyo ya Msimbazi hasa ikizingatiwa kwamba wachezaji wengine nao wamepewa sharti la kushinda mechi hiyo ili kuepuka adhabu kama iliyowakumba wenzao.
Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao, baadhi ya wachezaji wameelezea kuihofia mechi hiyo kuliko ilivyokuwa ile iliyowakutanisha na Yanga, iliyopigwa Oktoba 18 kwenye Uwanja wa Taifa na kumalizika kwa matokeo ya suluhu 0-0.
Kwa upande wao uongozi wa Mtibwa Sugar umewataka wenzao wa Simba kutumia busara kumaliza matatizo yao lakini wasiuchukulie mchezo wao kama kigezo cha kutimua wachezaji.
Kocha wa Mtibwa, Mecky Mexime aliliambia DIMBA kwamba, maandalizi yao na nia ya kutwaa ubingwa msimu huu ndiyo iliyowafikisha hapo na kwamba wana uhakika wa kushinda mechi yao dhidi ya Simba itakayopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
  Emmanuel Okwi (jezi nyekundu), mmoja wa wachezaji tegeemo kwa kikosi cha Patrick Phiri.

Yanga yafanya umafia Bukoba




 JUMA KASESA NA EZEKIEL TENDWA
YANGA SC imeifanyia umafia Kagera Sugar kwa kutanguliza kikosi kazi maalumu kwenda kuichunguza timu hiyo, kabla ya mchezo wao na timu hiyo Jumamosi wiki hii kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Kikosi cha kocha Mbrazil Marcio Maximo kinataka kuendeleza wimbi la ushindi ili kutimiza dhamira yao ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu unaoshikiliwa na Azam FC.
Kwa kutambua Kagera ni wagumu kufungika nyumbani, Yanga imefanya tena kile ilichokifanya msimu uliopita kwa kutuma kikosi kazi maalumu cha kuichunguza timu hiyo mbinu zake ili kurahisisha mipango yao ya kuondoka na pointi tatu Uwanja wa Kaitaba.
Msimu uliopita Yanga ilituma jopo la matajiri wakiongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, Stanley Katabaro ambaye ana asili ya Mkoa wa Kagera na baadhi ya wajumbe wenzake wa Kamati ya Utendaji kwenda kuichunguza timu hiyo na kuwasilisha taarifa muhimu kwa benchi la ufundi wakati huo likiwa chini ya kocha Fred Felix Minziro 'Majeshi'.
Na safari hii Yanga imetuma jopo la watu maalumu wa benchi la ufundi kwenda Wilaya ya Misenyi, ambako Kagera Sugar imejichimbia ikijifua chini ya kocha wake, Jackson Mayanja tayari kwa mchezo huo ambao ni gumzo kwa sasa.
Habari za uhakika kutoka ndani ya uongozi wa Yanga zimelieleza DIMBA Jumatano kwamba, jopo hilo limeshaingia Misenyi likiwachunguza wachezaji wa Kagera na limekuwa likiwasilisha taarifa kwa benchi la ufundi kila inapomalizika programu ya mazoezi ya timu hiyo.
Aidha, imeelezwa kikosi kazi hicho kilichopelekwa si rahisi kugundulika kwani Yanga imebaini ingempeleka tena Katabaro safari hii ingeweza kushtukiwa mpango wake mapema na Kagera.
Itakumbukwa Yanga ilikuwa haijapata ushindi uwanja huo tangu mwaka 2011 kabla ya kuvunja mwiko huo Oktoba 12, 2013 kwa kuichapa Kagera Sugar mabao 2-1.
Shukrani kwa mabao ya Mrisho Ngassa dakika ya 2 na Hamis Kiiza 'Diego' dk 60, yaliyoiwezesha timu hiyo kuondoka na ushindi kwenye uwanja huo.
Kikosi cha Yanga kimejichimbia Kahama kabla ya kuelekea Bukoba ambapo leo kinatarajiwa kucheza mchezo wa kujipima nguvu dhidi ya Ambassador FC ya mjini humo.
Maximo ameupania mchezo huo na ndio maana ameamua kusafiri na kikosi chake chote cha wachezaji 28 ambapo jana walijifua kikamilifu kuhakikisha wanarudi Dar es Salaam na ushindi mnono kutoka kwa wakata miwa hao wa Kagera.
Kikosi cha Maximo kitaingia kwenye mchezo huo kikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi mnono wa mabao 3-0 iliyoupata kwa Stand United mwishoni mwa wiki iliyopita wakati Kagera wao watakuwa na hasira ya kulazimishwa sare 1-1 nyumbani na 'Wagosi wa Kaya' Coastal Union.
Maximo amesema kwa sasa akili yake yote ni kuhakikisha hadondoshi pointi hata moja iwe ni Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam au viwanja vya mikoani yote hayo ikiwa ni kutimiza ahadi ya kuipa Yanga ubingwa.
Kocha huyo anajivunia kikosi kilichokamilika kila idara kuanzia golini hadi safu ya ushambuliaji ambapo hayo yote yalijidhihirisha katika mtanange dhidi ya Stand United walipopata ushindi mnono wa mabao 3-0 ambayo tangu ligi ianze msimu huu hawajawahi kuyafunga.
Jeuri kubwa aliyonayo Maximo ni kurudi kwa kiwango cha mshambuliaji wa timu hiyo, Jerryson Tegete alipofunga mabao mawili kwenye ushindi huo dhidi ya Stand huku lingine likifungwa na Mbrazil Geilson Santos ‘Jaja’.
Kazi kubwa iliyopo kwa Maximo ambayo inamfanya akune kichwa ni namna ya kuamua nani amuanzishe kikosi cha kwanza na nani abaki hasa kwenye safu ya ushambuliaji huku viungo nao wakipigana vikumbo kwa kuonyesha uwezo mkubwa.
Kutokana na kazi kubwa iliyoonyeshwa na Tegete kwa kufunga mabao mawili ni dhahiri kazi itakuwa kubwa kwa Jaja kuhakikisha anatetea nafasi yake hiyo ambapo pia Husein Javu pamoja na Nizar Khalfani nao wanakuja juu.
Kwa sasa kwenye kikosi cha Yanga, Tegete ndiye anayeongoza katika suala zima la upachikaji wa mabao mawili licha ya kwamba amecheza kwa dakika chache katika mchezo mmoja dhidi ya Stand United huku michezo yote minne akisugulishwa benchi.
Yanga wapo nafasi ya tatu wakiwa na pointi 10 sawa na Azam FC iliyopo nafasi ya pili huku Mtibwa Sugar wakiwa kileleni baada ya kujikusanyia pointi 13 timu zote zikiwa zimecheza mechi tano.
Kwa upande wao Kagera Sugar ambao watakuwa uwanja wao wa nyumbani kuwakabili Yanga, wapo katika nafasi ya saba na pointi sita ambapo mchezo wao huo unatabiriwa kuwa mkali kila timu ikihitaji kusogea mbele.