Tuesday, April 12, 2016

Yanga SC yapata dawa ya Waarabu



NA EZEKIEL TENDWA
KAMA ulidhani safari ya Yanga katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ndio imefikia tamati baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani, imekula kwako kwani Wanajangwani hao wamekuja na mbinu kali kuwamaliza Waarabu hao nyumbani kwao.
Unajua ikoje? Kocha Mkuu wa kikosi hicho Mholanzi, Hans Van De Pluijm, amechunguza kwa umakini kikosi chake na udhaifu uliojitokeza katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Taifa na sasa ndio anaufanyia kazi.
Katika mchezo wa kwanza uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Yanga walilazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na sasa Pluijm anataka kuishangaza Afrika kwa kuwaadhibu Waarabu hao tena wakiwa uwanja wao wa nyumbani.
Licha ya kwamba wadau wengi wa soka wanaamini Yanga wana mlima mrefu wa kupanda baada ya matokeo hayo ya sare Uwanja wa Taifa, kocha Pluijm alishaweka wazi kuwa kazi bado ni mbichi.
Pluijm ana uhakika wa kikosi chake kuibuka na ushindi katika mchezo huo hasa baada ya baadhi ya wachezaji wake waliokuwa majeruhi kama Mbuyu Twite kupona huku akiwa na uhakika wa kumtumia kiungo mwenye vitu vingi uwanjani, Haruna Niyonzima ambaye alikosa mchezo wa kwanza kutokana na kutumikia adhabu ya kadi mbili za njano.
Katika mchezo huo wa marudiano, Yanga watahitaji ushindi wowote ule au hata kutoka sare ya kufungana kuanzia mabao 2-2 lakini kama wakitoka sare ya bao 1-1 ni dhahiri timu hizo zitakwenda hatua ya kupigiana mikwaju ya penalti.
Kwa kulitambua hilo, Pluijm ameanza kuwaandaa wachezaji wake katika zoezi la upigaji penalti ambapo kwenye mazoezi ya jana yaliyofanyika viwanja vya Gymkana, kocha huyo alikuwa akiwapa mbinu za penalti.
Pluijm anakumbuka msimu wa 2014 ambao walitolewa na Al Ahly hao hao kwa mikwaju ya penalti na sasa hataki jambo hilo lijirudie tena kwani dhamira yake ni kuhakikisha msimu huu anawatia adabu Waarabu hao.
Waliopiga penalti hizo msimu huo wa 2014 na kukosa ni Oscar Joshua, Mbuyu Twitte, pamoja na Said Bahanuzi ambaye kama penalti yake ingeingia Yanga wangetinga moja kwa moja hatua inayofuata.
Waliopata penalti hizo walikuwa ni Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Didier Kavumbagu, pamoja na Emmanuel Okwi ambao hawapo kwa sasa katika kikosi hicho isipokuwa Cannavaro ambaye anaendelea kudunda.
Mbinu nyingine ambayo Wanajangwani hao watakwenda kuitumia ni kuhakikisha wanashambulia mwanzo mwisho kwani wanajua kuwa kitakachowaweka salama ni kuibuka na ushindi au kutoka sare ya zaidi ya mabao 2-2 vinginevyo watatupwa nje ya michuano hiyo.
Al Ahly, klabu inayoongoza kwa ubora barani Afrika ikiwa imetwaa ubingwa huo mara nane, inasaka ubingwa na kutaka kuendelea kuwa wafalme wa Afrika, hatua ambayo ndiyo itaingiza fedha zaidi kupitia kwenye matangazo na udhamini.
Yanga yenyewe inatafuta kufuzu kwa mara ya pili kwenye hatua ya makundi baada ya kufanya hivyo mwaka 1998, ambapo ilishika nafasi ya nne kwenye Kundi B na zawadi yake ya Dola 40,000 ikaishia mifukoni mwa wajanja wa kilichokuwa Chama cha Soka Tanzania (FAT). Licha ya Kamati ya Muda ya Tarimba Ghullam Abbas kupiga kelele, mpaka leo haijulikani ni nani hasa aliyefaidika nazo.
Licha ya kuwania Dola 400,000 hata kama itashika mkia kwenye kundi lake, lakini kushiriki hatua ya makundi kutaipa Yanga fursa ya kupata matangazo pamoja na kuongeza ubora wake barani Afrika.
Hata hivyo, Yanga ikifuzu hatua hiyo inaweza kuogelea kwenye utajiri mkubwa endapo itafanya vizuri pia, kwani zawadi zinatamanisha ambapo mshindi wa tatu kwenye kila kundi ataondoka na kitita cha Dola 500,000 (takribani Sh bilioni 1.05) wakati ambapo timu zitakazofuzu kucheza nusu fainali kila moja italamba Dola 700,000 (takribani Sh bilioni 1.47) ambao ni utajiri mkubwa unaoweza kusaidia kuweka mipango madhubuti ya kuendeleza klabu kwa kuimarisha programu ya soka la vijana.
Kwa mujibu wa CAF, bingwa wa mashindano hayo atajinyakulia kitita cha Dola milioni 1.5 (karibu Sh bilioni 3.15) huku mshindi wa pili akipata Dola milioni moja (Sh bilioni 2.1).
Hizi ni fedha nyingi, lakini haziwezi kuja kirahisi rahisi kwa sababu zinahitaji uwekezaji wa kutosha katika maandalizi ya timu pamoja na kuwa na mipango endelevu.
Kwa mujibu wa kanuni za CAF, hata kama Yanga itatolewa katika hatua hii, basi itaingia kwenye hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho kucheza na timu nane ambazo zitafuzu na ikishinda itaingia kuwania utajiri mwingine.
Katika kuhakikisha Waarabu hao wanatolewa katika michuano hiyo mchana kweupe, uongozi wa Yanga nao umeliunga mkono benchi la ufundi ambapo wameandaa kitita kikubwa cha fedha kwa ajili ya mchezo huo.
Taarifa za uhakika ambazo DIMBA imezinasa zinadai kuwa uongozi huo umeandaa milioni 220 ambazo ni kwa ajili ya usafiri kwa wachezaji na mashabiki wao pamoja na hoteli watakayofikia ikiwamo pia posho.
Taarifa hizo zinadai kuwa Wanajangwani hao hawataki kuhudumiwa kwa kitu chochote na wenyeji wao hao watakapofika huko Misri ili kuepuka aina yoyote ya hujuma ndiyo maana wameamua kujihudumia wenyewe kila kitu.

Wednesday, March 30, 2016

Habari njema kwa Wajasiriamali wadogo na wakati

Kutokana na mahitaji ya matangazo kuwa makubwa na baadhi ya watu hasa wenye kipato cha chini kushindwa kuyamudu, dirayaulimwengu imeamua kupunguza bei zake za matangazo madogo madogo hadi kufikia shilingi 35, 000/= kwa tangazo moja kwa wiki (siku saba).
Hivyo wajasiriamali na wale wenye biashara ndogo kama maduka ya nguo, maduka ya vyakula, wakulima, wauza vinywaji, wamiliki wa bar na night club, wamiliki wa shule au vyuo, wakati wao kuwafikia maelfu ya watu kupitia mtandao huu. Kwa wale wenye mahitaji wawasiliane na idara ya matangazo kwa simu namba 0784 890 387. 

RAIS MAGUFULI ATOA HATI YA KIWANJA KWA MSD



Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (kushoto), akimkabidhi hati ya kiwanja chenye ukubwa wa ekari tano Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu kilichotolewa na Rais Dk. John Magufuli kwa MSD kupitia Wizara hiyo Dar es Salaam leo mchana.Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu (kulia), akisalimiana Naibu Katibu Mkuu wa  Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Moses Kusiluka wakati wa hafla hiyo ya kukadhiana hati hiyo ya kiwanja. Katikati ni Waziri wa Wizara hiyo, William Lukuvi.
 Salamu zikiendelea. Hapa Mkurugenzi Mkuu wa MSD, akisalimiana na Mkurugenzi wa Mipango Miji, Profesa John Modestus.
 Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu (mbele kulia), akizungumza kwenye hafla hiyo.
 Waziri Lukuvi na Mkurugenzi wa MSD, wakiangalia hati hiyo.
Viongozi wa wizara hiyo wakiwa kwenye mkutano hafla hiyo. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Idara ya Usanifu Majengo, Amina Ramadhani, Ofisa Ardhi Mkuu, Mwamasage na Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani, Justo Lyamuya.

Na Dotto Mwaibale
RAIS Dk. John Magufuli kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi  ametoa kiwanja chenye ukubwa wa ekari 5 kwa Bohari ya Dawa (MSD) kilichopo Luguluni nje kidogo ya jiji la  Dar es Salaam, kwa ajili ya ujenzi wa Bohari ya Dawa ili kuondoa upotevu wa fedha kwa maghala ya kukodi.

Ujenzi wa maghala katika kiwanja hicho utaokoa kiasi cha sh. bilioni 4 zilizokuwa zikitumika kila mwaka kwa ajili ya malipo ya maghala ya kukodi yaliyopo Mabibo Ubungo jijini pamoja na kanda mbalimbali  nchini.

Akizungumza wakati wa akikabidhi hati hiyo kwa Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu Dar es Salaam leo mchana,  Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema, Rais ametoa ardhi hiyo ili kuepusha gharama zisizo na sababu kwa MSD.

Alisema agizo la rais fedha zilizokuwa zikitumika kwa ajili ya kukodi maghala hayo, zinapaswa kununua dawa ili kila Mtanzania apate huduma bora za kiafya.

“Rais aliniagiza niwape eneo, leo nimetekeleza agizo hilo kilichopo muanze ujenzi kama mlivyoomba kwa ajili ya kujenga ghala la dawa, naamini mtaanza mara moja balada ya kuendelea kukodi maghala na  badala yake fedha zote zitumike kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa tiba,” alisema Lukuvi na kuongeza;

“Kiwanja hiki ambacho kilikuwa cha Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) kilichokuwa na ukubwa wa ekari 200, tumewapa ekari tano kama uhitaji wenu ulivyokuwa, nimewasamehe kodi ya premium na badala yake kiasi cha Sh16.7 hamtalipa na gharama mtakayotakiwa kulipa ni sh. milioni 2 pekee ili muanze ujenzi mara moja.”

Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa  (MSD) Laurean Bwanakunu alisema tayari wameshazungumza na Bodi ya wadhamini, Wizara ya Afya na wahisani hivyo ujenzi unatarajiwa kuanza mara moja Julai Mosi.

“Tunamshukuru sana Rais kwa sababu ombi hili limefanyiwa kazi kwa haraka sisi kama MSD tulishindwa kuhimili mikiki kutokana na gharama kubwa iliyokuwa ikielekezwa katika malipo ya ghala la kukodi pale ubungo mwaka wa fedha ulioisha tulilipa kiasi cha Sh3.5 bilioni na tukitarajia mwaka huu mpya wa fedha inafikia Sh4 bilioni kwa sababu ya malipo kwa dola,” alisema Bwanakunu.

Alisema katika eneo hilo jipya lililopo Luguluni wanatarajia kujenga zaidi ya maghala matano yenye ukubwa wa sikwea mita mita 5000 yatakayogharimu kiasi cha sh. bilioni 10nkila mojawapo, “ujenzi huu utakapokamilika kanda zitakazonufaika ni pamoja na Dar es Salaam, Morogoro na Pwani na kuwa eneo hilo walilopata wanaweza kujenga kiwanda cha maji. (Imeandaliwa na Dotto Mwaibale)

Msuva ampa Tambwe kiatu cha dhahabu

NA ZAINAB IDDY
LICHA ya mshambuliaji wa Simba, Hamis Kiiza, kuongoza katika mbio za ufungaji bora, mfungaji bora wa msimu uliopita, Simon Msuva wa Yanga, amesema kwamba Mrundi, Amis Tambwe, ndiye atakayeibuka mfungaji bora msimu huu.
Msuva amelisema kwamba, licha ya Tambwe kupata upinzani mkali kutoka kwa Kiiza, lakini ana nafasi kubwa ya kupata tuzo hiyo msimu huu kutokana na uwezo wake wa kupachika mabao.
 “Najua upinzani katika mbio hizo za ufungaji bora ni mkubwa lakini kwangu mimi nampa nafasi kubwa Tambwe kwani anao uwezo mkubwa wa kutumia nafasi anazozipata,” alisema Msuva.
Tambwe ambaye msimu wa 2013/14 aliibuka mfungaji bora akiwa na mabao 17 wakati huo akiichezea Simba, kwa sasa ana mabao 17, nyuma ya Kiiza mwenye mabao 19.
Katika msimu uliopita, Msuva alifanikiwa kutwaa tuzo ya ufungaji bora baada ya kuifungia timu yake jumla ya mabao 17 akifuatiwa na Tambwe aliyetikisa nyavu mara 15.

Azam macho yote kwa Prisons kesho

NA SALMA MPELI
UONGOZI wa timu ya Azam FC umesema kuwa kwa sasa macho yao yote yapo kwa Tanzania Prisons ambao wanatarajia kukutana nao kesho ikiwa ni mechi ya Kombe la Shirikisho (FA) mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Akizungumza na DIMBA, Ofisa Habari wa Azam, Jafari Idd, alisema hiyo ndiyo mechi iliyoko mbele yao kwa sasa kabla ya ile ya ligi dhidi ya Toto African ya Mwanza, Aprili 3 kabla ya kukutana na Esperance ya Tunisia kwenye Kombe la Shirikisho.
“Tunajiandaa kuhakikisha tunaibuka na ushindi ili kuingia hatua ya nusu fainali, tunashukuru kikosi chetu kimekamilika baada ya wachezaji wa timu ya Taifa kurejea na kujiunga kambini pamoja na wenzao,” alisema Jaffer.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Azam wapo nafasi ya tatu wakiwa na pointi 50 sawa na Yanga huku zikitofautiana idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

African Sports kusaka kocha Zanzibar

NA SALMA MPELI
UONGOZI wa African Sports ya Tanga upo katika harakati ya kumsaka kocha kutoka visiwani Zanzibar atakayeziba nafasi ya Ramadhan Aluko aliyefukuzwa hivi karibuni.
Akizungumza na DIMBA, Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, Abdul Bosnia, alisema wanahitaji kocha kwa haraka na tayari wapo katika mchakato huo kwa ajili ya kuanza kazi mapema ili kuinusuru timu kutoka kwenye hatari ya kushuka daraja.
“Tunahitaji kocha kwa haraka baada ya kuamua kuachana na Aluko, tumelenga kutafuta mwalimu kutoka Unguja ili aanze kazi mapema,” alisema.
African Sports ipo nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na jumla ya pointi 20 juu ya ndugu zao Coastal Union ambao wanaburuza mkia wakiwa na pointi 19 ambapo timu hizo zote zipo kwenye hatari ya kushuka daraja.
Timu hiyo ilipanda daraja msimu uliopita na kuanza kucheza Ligi Kuu msimu huu baada ya kucheza ligi hiyo kwa mara ya mwisho mwaka 1988, lakini hata hivyo mashabiki wao wana wasiwasi mkubwa kutokana na majaliwa na timu hiyo katika msimu ujao wa ligi kwani huenda isiwepo msimu ujao.


Manara: Al Ahly iifunge Yanga 5-0

NA EZEKIEL TENDWA
UNAKUMBUKA yale mabao 5-0 ambayo Simba waliwafunga Yanga msimu wa 2012? Sasa ni hivi, msemaji wa Wanamsimbazi hao, Haji Manara, amesema anataka Al Ahly iibuke na ushindi kama huo dhidi ya Wanajangwani hao Jumamosi ya Aprili 9.
Unajua kwanini Manara ameamua kutamka maneno hayo? Jibu ni jepesi tu kwamba kama Yanga wataibuka na ushindi dhidi ya Al Ahly katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jiji halitakalika.
“Nataka Yanga ifungwe mabao 5-0 kama tuliowafunga sisi mwaka 2012 kwani hawa Yanga wakishinda mji hautakalika. Nadhani ikiwa hivi mambo yatakuwa sawa sawa na mji utakalika na kahawa itanyweka,” alisema Manara mtoto wa nyota wa zamani wa Yanga, Sunday Mnara ‘Computer’.
Yanga na Al Ahly zinatarajiwa kukutana Aprili 9 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, mchezo wa mabingwa barani Afrika.