Wednesday, April 29, 2015

Ngassa afichua siri ya ubingwa Jangwani

NA ZAINAB IDDY
WINGA wa kutegemewa wa mabingwa wapya wa Ligi Kuu Tanzania Bara (Yanga), Mrisho Khalfani Ngassa 'Anko,' amefichua siri ya timu hiyo kutwaa ubingwa msimu huu kuwa ni uwepo wa benchi la ufundi lenye weledi wa soka.
Yanga juzi iliweza kutangaza ubingwa baada ya kuifunga Polisi Morogoro mabao 4-1 na kufikisha jumla ya pointi 55, ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote hata mabingwa wa msimu uliopita, Azam FC waliopo nafasi ya pili na pointi 45 katika msimamo wa ligi hiyo.
Ngassa ameliambia DIMBA Jumatano kuwa mafanikio ya kikosi chao yanatokana na ujuzi wa makocha wao.
Ngassa alisema pongezi nyingi zinastahili kwenda kwa makocha Hans  van der Pluijm  pamoja na msaidizi wake, Charles Mkwassa, ambao wameweza kuwaweka wachezaji kuwa kitu kimoja na hamasa wanazozitoa pindi kikosi kinapopata matokeo mazuri  au mabaya ndizo zilizochangia kujituma kwa kila mmoja wao.
Alisema licha ya mchezaji mmoja mmoja kujitengenezea jina katika soka la Tanzania, lakini  kocha ndiye nguzo muhimu kwao katika kuhakikisha matokeo bora yanapatikana.
"Kama inavyokuwa timu ikifanya vibaya mzigo wa lawama wanabebeshwa makocha, basi hata ubingwa wetu msimu huu wao ndiyo wanastahili pongezi nyingi kutokana na jitihada zao binafsi za kutumia akili za ziada ili kuhakikisha kikosi kinakuwa cha ushindani pasipo kujali changamoto za ligi yenyewe.
"Walihakikisha tunakuwa kitu kimoja, tunajituma kila mmoja kwa nafasi yake, huku  wakipigania kuona tunapata kila kinachohitajika kwa mchezaji ili aweze kufanya kazi yake kwa moyo mmoja, hizo ni juhudi kubwa ambazo si makocha wote wanaweza kuzifanya,"  alisema.
Hadi sasa Yanga imefanikiwa kutwaa kombe la Ligi Kuu Tanzania Bara mara 25 na kushikilia rekodi ya kuwa mabingwa mara nyingi zaidi, wakifuatiwa na Simba waliolinyakua mara 19.

Goran aibadilishia kikosi Azam

NA MWANDISHI WETU
KOCHA Mkuu wa Simba, Goran Kopunovic, ameamua kubadili kikosi chake ili aweze kuifanyia kitu mbaya Azam FC katika mchezo utakaozikutanisha timu hizo wikiendi hii kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Simba na Azam zitapambana Jumapili kuwania kuweka sawa mipango ya kushika nafasi ya pili, ili kupata tiketi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
Azam wapo nafasi ya pili wakiwa na pointi 45, Simba wakiwa nyuma yao katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 41, wakibakiwa na michezo miwili, huku wakiwaombea mabaya Wanalambalamba hao wapoteze michezo yao mitatu ili wawapiku.
Kama Simba watashinda michezo yao hiyo miwili dhidi ya Azam na JKT Ruvu na Wanalambalamba hao wakafanya vibaya michezo yao, ikiwamo huo wa Simba, Yanga pamoja na Mgambo JKT itawapa fursa ya kumaliza nafasi ya pili.
Kutokana na hali hiyo, Kocha Mkuu wa Simba, Goran Kopunovic, ameanza kuzichanga vema karata zake ili kuhakikisha anawashushia kipigo Azam FC na baadaye kumalizia kwa maafande wa JKT Ruvu.
Akizungumza na DIMBA Jumatano, Kopunovic alisema, anaangalia uwezekano wa kubadili kikosi chake kwa namna ambavyo anajua yeye, ili kuwachanganya wapinzani wake na kupata kile ambacho amekikusudia.
"Kila kitu kinakwenda vizuri, naamini kwa jinsi nitakavyokipanga kikosi changu tutafikia malengo yetu, kilichopo ni kila Mwanasimba kujitolea kwa hali yoyote," alisema.

Tambwe aweka rekodi ya kutisha Ligi Kuu

Na Mwandishi Wetu
STRAIKA wa Yanga, raia wa Burundi, Amissi Tambwe, ameweka bonge la rekodi ya kutisha kwa kuwa mchezaji wa kwanza kupiga hat-trick (mabao matatu mechi moja) ya pili msimu huu, ikiwa ni ya nne kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Mrundi huyo ni mchezaji pekee aliyeweka rekodi hiyo ambayo haijawahi kuwekwa na mchezaji yeyote tangu uwanja huo ulipoanza kutumika.
Mechi ya kwanza kwa straika huyo kufunga hat trick kwenye uwanja huo ilikuwa ni Februari Mosi, 2014, dhidi ya JKT Oljoro, akiwa na Simba, ambayo ilishinda 4-0.
Mechi nyingine ambayo Mrundi huyo alifunga hat trick ilikuwa ni Septemba 19, 2014 dhidi ya Mgambo JKT, ambayo timu yake ya Simba ilipata ushindi mnono wa mabao 6-0.
Mshambuliaji huyo alikamilisha rekodi yake ya kupiga hat-trick ya tatu Aprili 8, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, kwa kufunga mabao manne katika ushindi wa mabao 8-0 dhidi ya Coastal Union, iliyocheza na Yanga.

Tambwe, aliyekuwa mfungaji bora msimu uliopita wa ligi kuu, akifunga mabao 19, alitua kuichezea Yanga kwenye usajili wa dirisha dogo msimu huu akitokea Simba, baada ya kumsitishia mkataba wake kabla ya kutua Jangwani.
Upo uwezekano mkubwa wa mshambuliaji huyo kukitetea kiatu chake cha dhahabu kutokana na kasi yake kubwa aliyonayo hivi sasa ya kufunga mabao.
Mrundi huyo, hadi hivi sasa amefanikiwa kufunga mabao 14, akiongozwa na Simon Msuva mwenye 17, akifuatiwa na mshambuliaji wa Azam FC, Didier Kavumbagu aliyepachika 10 na Rashid Mandawa wa Kagera Sugar ambaye naye ana mabao 10.
Kati ya hat-trick hizo alizozipiga, idadi kubwa ya mabao amefunga kwa kichwa, kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufunga aina hiyo ya mabao, huku mengine akifunga kwa kumchambua kipa.

Wednesday, April 22, 2015

Mechi nne kuondoka na watu Simba


NA EZEKIEL TENDWA
WAKATI Simba ikiwa imebakisha michezo minne ikianzia na wa leo dhidi ya Mgambo JKT kumaliza Ligi  Kuu Tanzania Bara, wachezaji wa timu hiyo watacheza kwa tahadhari kubwa kuepuka panga la usajili mara Ligi hiyo itakapofikia tamati Mei, mwaka huu.
Simba wapo nafasi ya tatu wakiwa na pointi zao 35, nyuma ya Azam wenye pointi 42, kila timu ikiwa imecheza michezo 22, zikibakiwa na michezo minne kumalizia Ligi hiyo ambapo kila moja ikiapa kushinda michezo yake yote.
Ili Simba wamalize nafasi ya pili, wanatakiwa washinde michezo yao yote minne iliyobaki, ukiwamo dhidi ya Azam FC, huku wakiwaombea Wanalambalamba hao kupoteza angalau michezi mitatu kati ya minne waliyobakiwa nayo.
Kocha Mkuu wa Simba, Goran Kopunovic, ameweka wazi kuwa bado ana matumaini ya kikosi chake kumaliza katika nafasi ya pili, huku akitamba kuibuka na ushindi mnono dhidi ya maafande hao wa Mgambo leo, ili kuzidi kuwasogelea Azam.
Ukiacha mchezo wa leo, Simba imesaliwa na mechi dhidi ya Azam FC, Ndanda FC na  JKT Ruvu.
Michezo yote hiyo Simba wataicheza katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, huku wapenzi na mashabiki wao wakiwa na hamu ya kuona kikosi hicho kinashinda michezo hiyo ili kujiweka katika mazingira ya kupata nafasi ya kucheza michuano ya kimataifa mwakani, huku wakiwaombea mabaya Azam FC.
Habari za uhakika ambazo Dimba Jumatano inazo ni kwamba, baadhi ya wachezaji ambao wamesajiliwa kwa bei kubwa na kushindwa kuonyesha cheche zao wapo kwenye wakati mgumu wa kama wataendelea kuwepo kwenye kikosi hicho msimu ujao au kutemwa.
Wachezaji wa Kimataifa, Danny Sserunkuma pamoja na Simon Sserunkuma wapo kwenye mtihani mgumu, kutokana na kusajiliwa kwa bei kubwa huku wakishindwa kufanya mambo ya kulikuna benchi la ufundi.


Nyota ya Ngassa yazidi kung’aa Afrika


NA SHARIFA MMASI
WAKATI winga wa Yanga, Mrisho Ngassa akiwa amemaliza mkataba wake ndani ya kikosi hicho, nyota yake imezidi kung’aa barani Afrika, baada ya klabu kadhaa kuonyesha kukunwa na kiwango chake, hivyo kuitaka saini yake kwa udi na uvumba.
Awali Ngassa alishafanya mazungumzo na kusaini mkataba wa awali na timu ya Free State ya Afrika Kusini, lakini moja ya timu kubwa ya nchini Qatar pia imeonyesha nia ya kumhitaji kabla ya Etoile du Sahel ya Tunisia nayo kufunguka juu ya mchezaji huyo.
Habari za uhakika ambazo DIMBA Jumatano imezipata zinaeleza kuwa, mbali na timu hizo, pia klabu ya AS Vita ya Congo  DRC nayo inahitaji saini ya winga huyo, huku klabu yake, Yanga nao wakihaha kumshawishi kumpa mkataba mpya baada ya kuwafanyia mambo kwenye Ligi Kuu na michuano ya kimataifa.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro, amekiri Ngassa kumaliza mkataba wake na klabu hiyo na kusema suala la mchezaji huyo kutamaniwa na timu mbalimbali barani Afrika kwa sasa halina nafasi kwao, kwani kila kitu kitawekwa wazi baada ya ligi kumalizika Mei, mwaka huu.
"Ni kweli kwamba Ngassa amemaliza mkataba wake, lakini kama mnavyomwona anaendelea kuichezea Yanga hivyo tunawaomba mashabiki wetu wala wasiwe na wasiwasi juu ya jambo hilo, kwani uongozi wao upo makini," alisema Muro.


Simba yamtengea Msuva Ml. 170

NA SAADA SALIM
KAMATI ya Usajili ya Klabu ya Simba imetenga Sh milioni 170 kwa ajili ya kumnasa winga machachari wa Yanga, Simon Msuva, ili aisaidie timu hiyo katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu ujao.

Taarifa zisizo na shaka zilizolifikia DIMBA Jumatano kutoka kwa kigogo mmoja wa Kamati hiyo zinaeleza kuwa tayari wameshatenga donge hilo kwa ajili ya kumnasa Msuva, ambaye amekuwa na msimu mzuri ndani ya Yanga kutokana na kuwa mwiba mkali wa kucheka na nyavu.
"Suala la Msuva kuja Simba halina ubishi wowote, kwani Kamati inaendelea na harakati za kumnasa winga huyo kwa ajili ya msimu ujao," alisema kigogo huyo na kuongeza: "Dau hilo tulilomtengea tuna uhakika kabisa hawezi kulikataa".
Kwa nyakati tofauti Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Kepteni Zacharia Hanspope, amekiri uwepo wa mpango wa kuipa pigo Yanga kwa kumchukua Msuva kwa madai kuwa kiwango chake ni kizuri na pia hata yeye mwenyewe anaipenda Simba, hivyo hawana budi kumrejesha nyumbani.